Berlin, Ujerumani
Klabu ya Bayern Munich imemfuta kazi kocha wake, Julian Nagelsmann na kumteua kocha wa zamani wa Chelsea, Thomas Tuchel kushika wadhifa huo kazi ambayo ataianza rasmi Jumatatu hii.
Hatua ya kumtimua Nagelsmann imekuja baada ya mwenendo wa timu kutowaridhisha mabosi wa klabu hiyo wakati huu timu hiyo ikiwa nafasi ya pili katika Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga.
Mabosi Bayern wamechukua uamuzi wa kumfukuza Nagelsmann katika kipindi ambacho timu hiyo inajiandaa kwa mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Man City na mechi ya Bundesliga dhidi ya mahasimu wao, Borussia Dortmund itakayopigwa Aprili Mosi.
Hivi karibuni chanzo kimoja cha habari kiliripoti kuwapo mpango wa kumtimua, Nagelsmann huku jina la Tuchel likichomoza miongoni mwa makocha waliopewa nafasi kubwa kupewa kibarua hicho.
“Bayern imemfuta kazi Julian Nagelsmann, uamuzi umechukuliwa na ofisa mtendaji mkuu, Oliver Kahn na mjumbe a bodi anayehusika na michezo, Hasan Salihamidzic baada ya mazungumzo na rais wa klabu, Herbert Hainer,” ilieleza taarifa ya Bayern.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Tuchel sasa atafanya kazi ya kuinoa timu hiyo kwa mkataba utakaofikia ukomo Juni 30, 2025 na Jumatatu ataanza rasmi kuongoza mazoezi ya timu hiyo.
Pamoja na Nagelsmann, wengine waliofutwa kazi ni makocha wasaidizi, Benjamin Gluck, Dino Toppmoller na Xaver Zembrod.
Nagelsmann aliajiriwa na Bayern Aprili, 2021 na kuiongoza timu hiyo msimu uliopita hadi kutwaa taji lake la 10 mfulululizo la Bundesliga na kumaliza ligi ikiwa mbele kwa pointi nane dhidi ya Dortmund walioshika nafasi ya pili.
Bayern hata hivyo mambo si mazuri msimu huu ikiwamo kipigo cha hivi karibuni cha mabao 2-1 mbele ya Bayer Leverkusen, kipigo ambacho kiliisaidia Dortmund kushika usukani kwenye Bundesliga.
