Paris, Ufaransa
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps (pichani) ameupinga msimamo wa Fifa wa kuzipa nchi sita uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2030 akihoji mantiki ya uamuzi huo kwenye mchezo wa soka.
Fifa ilitangaza kuwa mwaka 2030 fainali za Kombe la Dunia zitachezwa katika nchi sita za mabara matatu kama njia mojawapao ya kusherehekea miaka 100 tangu kuanzishwa kwa fainali hizo.
“Ukiacha mbali ukweli kwamba ni jambo la kawaida kuandaa fainali katika nchi zaidi ya moja lakini sasa kuna mechi tatu kuchezwa Marekani ya Kuisni,” alisema Deschamps katika mkutano na waandishi wa habari wakati timu yake ikijiandaa kwa mechi ya kufuzu Euro 2024.
“Sijui ni nchi gani zitakazohusika na hilo lakini maana yake ni kwamba nchi za Marekani ya Kusini zitakuwa na faida na nchi nyingine zitalazimika kusafiri na kusafiri zaidi,” alisema.
“Sijui ni nani anayefanya maamuzi lakini siwezi kuwaficha ukweli kwamba huwa napenda mambo yaliyo kwenye utaratibu mzuri na sidhani kama mambo hayo yapo kwenye uamuzi huo,” alisema Deschamp ambaye timu yake inaongoza Kundi B katika mbio za kuwania kufuzu Euro 2024.
Jumatano iliyopita Fifa ilizitangaza nchi za Morocco, Ureno na Hispania kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2030 lakini pia ikatoa fursa kwa nchi za Argentina, Paraguay na Uruguay kuwa wenyeji wa mechi tatu.
Mechi ya kwanza ya fainali za 2030 itapigwa kwenye dimba la Centenario ambapo ndipo mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia 1930 ilichezwa.
Kwa uamuzi huo wa Fifa maana yake ni kwamba nchi zote sita ambazo zimeteuliwa kuwa wenyeji wa fainali za 2030 zitafuzu moja kwa moja fainali hizo zitakazoshirikisha jumla ya timu 48.