Na mwandishi wetu
Pazia la Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-24 litafungiliwa Agosti 16 kwa mabingwa watetezi Yanga kurusha karata ya kwanza Agosti 23 dhidi ya KMC wakati Simba wataianza ligi Agosti 17 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Stephen Mguto, Agosti 16 ambayo ndiyo siku ya ufunguzi wa ligi hiyo zitapigwa mechi tatu; Ihefu itaumana na Geita Gold, Namungo dhidi ya JKT Tanzania na Dodoma Jiji dhidi ya Coastal Union.
Ukiacha mechi ya Simba na Mtibwa ya Agosti 17, siku hiyo pia kutakuwa na mechi kati ya Singida Fountain Gate itakayotoana jasho na Tanzania Prisons wakati Simba watarudi uwanjani kwa mara ya pili Agosti 20 kuoneshana kazi na Dodoma Jiji.
Siku tisa baada ya Simba kucheza mchezo wa pili yaani Agosti 29, mahasimu wao Yanga wataingia dimbani dhidi ya JKT Tanzania wakati siku moja kabla yaani Agosti 28, Azam watakuwa dimbani dhidi ya Tanzania Prisons.
Kati ya Oktoba 4 hadi 19, ligi itasimama kupisha michuano ya kimataifa kwa timu za Yanga, Simba, Azam na Singida Fountain Gate zitakazokuwa zikiumana kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa upande wa Simba wanatarajia kukosekana kwa kipindi kirefu cha mwezi Oktoba kwa kuwa mbali na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo pia itashiriki michuano mipya ya Africa Super Cup.
Baada ya mtihani huo, Simba itakuwa na kazi nyingine mapema Novemba 5 itakapokutana na hasimu wake wa jadi Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Mkapa Simba ikiwa mwenyeji.
Timu hizo mbili mahasimu, mechi hiyo inaweza kuwa ya pili kwa msimu huu kama ikitokea zikakutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii inayoshirikisha timu za Yanga, Simba, Azam na Singida Fountain Gate.
Kwa mujibu wa Mguto, ligi hiyo imepangwa kufikia tamati Mei 29, 2024 kwa mechi zote kuchezwa siku hiyo.
Soka Ligi Kuu NBC Agosti 16
Ligi Kuu NBC Agosti 16
Read also
