Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG), Kylian Mbappe ameanza mazoezi tayari kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich itakayopigwa leo Jumanne usiku.
Hali pia ni hivyo hivyo kwa nyota mwingine wa timu hiyo, Lionel Messi ambaye baada ya kuwa majeruhi, hatimaye ameshiriki mazoezi ya jana Jumatatu na leo Jumanne anatarajiwa kuwa dimbani.
PSG na Bayern zitaumana leo usiku katika mechi ya hatua ya 16 bora, ambayo awali ilitarajiwa Mbappe angeikosa baada ya kuumia misuli na kuelezwa kuwa angekuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Baada ya kufanya mazoezi yapo matumaini kuwa mchezaji huyo yuko vizuri na huenda leo akawa uwanjani dhidi ya Bayern, mechi inayowakumbusha mashabiki tukio la fainali ya Ligi ya Mabingwa 2020 ambapo timu hizo zilikutana na Bayern kushinda kwa bao 1-0.
“Bado hatuna uhakika kama atakuwa kwenye orodha ya wachezaji watakaocheza, Kylian alifanya mazoezi kwa vipindi vyote leo (jana Jumatatu) tuliamua afanye mazoezi na wachezaji wote,” alisema kocha wa PSG, Christophe Galtier jana.
Kocha Galtier pia alisema kwamba Messi naye ambaye pia alikuwa na matatizo ya misuli alipata matibabu na yumo katika kikosi cha PSG kitakachovaana na Bayern.
Kama Mbappe na Messi wote watarudi uwanjani, wanatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa PSG ambayo ilipoteza mechi zake mbili zilizopita za ndani.