Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amesema mchezo wao dhidi ya Wydad AC ni fainali kwao kwani ndio ulioshikilia hatma yao kwenye kundi.
Simba wako mkiani mwa kundi B wakiwa na pointi mbili baada ya kushuka uwanjani mara tatu wakiwa wamepata sare mbili na kupoteza mchezo mmoja, hivyo kuwa timu pekee ambayo haijashinda kwenye kundi lake.
Akizungumza leo Jumatatu, Benchikha alisema matumaini yao yamebaki kwenye mchezo wa Desemba 19, mwaka huu ambao kwao ndio fainali ya kwanza wanayopaswa kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kwenye kundi.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu tunapaswa kushinda, tuna pointi mbili hivyo kama tutapoteza tutakuwa tumebaki palepale hivyo tunahitaji kushinda ili kujiweka sehemu salama.
“Nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi waje kutupa sapoti tunaenda kucheza na timu bora lakini tunapaswa kushinda ili kuweka mahesabu yetu sawa kwenye kundi,” alisema Benchikha.
Benchikha pia alisema kuwa bado wana tatizo kwenye safu ya ushambuliaji kwani wanapaswa kuwa watulivu.
“Wanafanya kazi kubwa lakini wanashindwa kufunga bao, katika michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Asec Mimosas, Jwaneng Galaxy na Wydad Casablanca hivyo tuna kazi ya kufanya,” alisema.