Na mwandishi wetu
APR ya Rwanda imefuta matarajio ya Yanga kukutana na hasimu wake Simba katika Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Amaan Complex.
Katika siku za karibuni viongozi na mashabiki wa Yanga wamekuwa wakijitapa kuwa na hamu ya kukutana na Simba katika michuano hiyo lakini mechi ya leo Jumapili imefuta ndoto hizo.
Kwa ushindi huo, APR mbali na kuifanya Yanga iwe kama vile imekacha kucheza Dar Derby na Simba, timu hiyo pia inakuwa imefuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 23 lililofungwa na Jesus Moloko kwa shuti kali baada ya kuinasa pasi ya Clement Mzize aliyemzidi kasi beki mmoja wa APR.
Matarajio ya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao hilo moja yalizimwa katika dakika tatu za nyongeza baada ya APR kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Souley Sanda aliyeuwahi mpira uliopigwa na Victor Mbaoma na kutemwa na kipa wa Yanga, Abutwalib Mshery.
Dakika nne baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, APR waliandika bao la pili lililofungwa na Mbaomwa kwa mkwaju wa penalti.
Juhudi za Yanga kutaka kusawazisha bao hilo zilizimwa dakika ya 62 baada ya APR kuandika bao la tatu na la ushindi lililofungwa na Sharaf Shaiboub ambaye aliitumia pasi ya kisigino aliyounganishiwa na Taiba Mbonyumwami.
APR sasa inasubiri kuumana na mabingwa watetezi, Mlandege katika mechi ya nusu fainali, baada ya Mlandege kushinda mechi yake ya robo fainali dhidi ya KVZ kwa mikwaju ya penalti 3-2.
Soka APR yaifuta Dar Derby, yailaza Yanga 3-1
APR yaifuta Dar Derby, yailaza Yanga 3-1
Read also