Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa Barca, Dani Alves anayekabiliwa na kesi ya kumdhalilisha mwanamke ataendelea kusota rumande kwa mwezi wa tano sasa baada ya mahakama kukataa ombi lake la kutaka apewe dhamana.
Alves alikamatwa Januari mwaka huu akituhumiwa kumdhalilisha mwanamke katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona na tangu wakati huo ameendelea kusota rumande wakati uchunguzi ukiendelea.
Hati za kusafiria za mchezaji huyo za Brazil na Hispania zinashikiliwa na mahakama hiyo ya mjini Barcelona ingawa Alves mwenyewe amekuwa akisisitiza kwamba hajafanya kosa lolote .
Mara ya kwanza mchezaji huyo kuomba apewe dhamana ilikuwa ni miezi miwili iliyopita ambapo alikataliwa kwa kilichodaiwa kwamba mtuhumiwa huyo anaweza kutoroka.
Mahakama hiyo imesisitiza kwa mara nyingine jana Jumanne kwamba mchezaji huyo ambaye pia amewahi kuchezea kwa mafanikio makubwa klabu kadhaa kubwa na maarufu za Ulaya kutokana na utajiri alionao anaweza kutoroka wakati wowote.
Mara baada ya sakata la mchezaji huyo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na Alves kuwekwa rumande, klabu anayoichezea sasa ya Pumas UNAM ya Mexico nayo ilitangaza kumfutia mkataba.
Akiwa katika ubora wake kwenye soka, kati ya mwaka 2008 na 2016, Alves ameichezea Barca mechi 408 na kushinda mataji sita ya La Liga na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini pia amewahi kuzichezea timu za Juventus na PSG hapo hapo akiichezea timu ya Taifa ya Brazil mara 126.
Kimataifa Alves aendelea kusota rumande
Alves aendelea kusota rumande
Read also