Paris, Ufaransa
Kocha wa PSG, Luis Enrique amekana na kuziita uwongo habari zinazodai kwamba alitukanwa na mshambuliaji wake, Kylian Mbappe baada ya kocha huyo kumtupa benchi katika mechi dhidi ya Marseille.
Mbappe alionekana mwenye sura ya hasira wakati akielekea kwenye benchi na kuonekana kama akitoa kauli ambayo baadhi ya mitandao ya kijamii iliitafsiri kuwa ni kauli za kumtukana Enrique.
Katika mechi baina ya timu hizo mahasimu iliyopigwa Jumapili iliyopita, PSG ilitoka na ushindi wa mabao 2-0 ingawa baada ya hapo tukio la Mbappe kutupwa benchi liligeuka mjadala.
“Jambo la msingi ni kwamba kila kitu kinachotengenezwa kutokana na uwongo ni katika yale mambo yanayotokea kwenye dunia ya soka, kuna mmoja ametengeneza mtu kutukanwa na uvumi wa kila aina ulioibuka,” alisema Enriqque.
Katika mechi saba zilizopita za PSG kwenye Ligi 1, Mbappe amecheza moja tu kwa dakika zote 90 ambapo Enrique amekuwa akimuweka benchi kwa kumuingiza kipindi cha pili au kumtoa wakati mechi ikiendelea.
Enrique amechukua uamuzi huo tangu Mbappe atangaze Februari mwaka huu uamuzi wake wa kuihama timu hiyo baada ya msimu huu huku habari zikidai kwamba mazungumzo kati yake na klabu ya Real Madrid yanaendelea.
Katika siku za karibuni, Enrique alisema kwamba anaamini mchezaji huyo atabadili maamuzi na kubaki PSG ingawa kabla ya hapo alisema kwamba ni lazima wajiandae na maisha bila ya Mbappe na hapo hapo akaanza utaratibu wa kumtupa benchi.
Kocha huyo pia alimsifia mchezaji huyo kwa ubora wake pamoja na wachezaji wote wa PSG mara baada ya mechi na Marseille na kuongeza kuwa Mbappe alikuwa na tabia njema.
Kimataifa Kocha PSG akana, Mbappe hajamtukana
Kocha PSG akana, Mbappe hajamtukana
Read also