Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kumuondoa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na wasaidizi wake na nafasi yake sasa itashikwa na Hanour Janza atakayesaidiwa na Mecky Maxime wakati kipa mkongwe Juma Kaseja akipewa jukumu la kuwanoa makipa wa timu hiyo.
Taarifa ya TFF iliyopatikana leo na kusainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa leo baada ya pande mbili yaani TFF na Poulsen kufikia makubaliano kwenye kikao cha pamoja ambapo kwa sasa Poulsen atabaki kwenye timu za vijana hadi mkataba wake utakapofikia ukomo.
Na ingawa taarifa ya TFF haikueleza nini hasa sababu za kufikia uamuzi wa kuachana na kocha huyo, inaaminika kuwa matokeo mabaya ya hivi karibuni huenda yatakuwa yamechangia kufikia uamuzi wa kuachana na kocha huyo raia wa Denmark.
Stars kwa sasa ipo katika mbio za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) ambapo imekuwa ikisuasua kwa kupata matokeo yasiyoridhisha, ilianza kwa kupata ushindi mdogo wa bao 1-0 dhidi ya timu inayotajwa kuwa dhaifu ya Somalia kabla ya kushinda kwa mabao 2-1 katika mechi ya marudiano, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Matokeo hayo yaliiwezesha Stars kusonga mbele na kukutana na Uganda Cranes ambapo jana ilijikuta ikilala nyumbani kwa bao 1-0 na hivyo kujiweka katika wakati mgumu kwenye mechi ya marudiano inayotarajiwa kuchezwa wikiendi hii ambapo Stars itakuwa ugenini.
Kimataifa Kim Poulsen aondolewa Stars
Kim Poulsen aondolewa Stars
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
