London, England
Cristiano Ronaldo hayumo katika kikosi cha wachezaji wa Manchester United ambao wameondoka jioni ya leo kuelekea Bangkok, Thailand kwa ziara ya maandalizi ya msimu wa 2022/23.
Ronaldo hajajiunga na wachezaji wenzake katika kikosi cha timu hiyo kwa kile kilichoelezwa awali kwamba ni majukumu ya kifamilia lakini ilitarajiwa angekuwamo katika ziara hiyo ya wiki mbili inayoanza leo na baada ya Thailand kikosi hicho kitaelekea nchini Australia.
Taarifa ya klabu hiyo imeeleza kuwa mchezaji huyo ameongezewa muda wa mapumziko ili aendelea kuweka sawa mambo ya kifamilia kwani hapo kabla alitakiwa kuripoti kambini Jumatatu, “Cristiano Ronaldo hatokuwa sehemu ya wachezaji wanaokwenda Thailand kwa kuwa ameongezewa siku za mapumziko ili kuweka sawa mambo yake ya kifamilia.”
Haijaweza kueleweka mara moja kama bado matatizo ya kifamilia yanamkabili mchezaji huyo ambaye pia haijaelezwa ni lini anatakiwa kuripoti kambini lakini kilichopo ni kwamba ameshaonyesha nia ya kutaka kuachana na klabu hiyo jambo linaloonekana kuwa gumu kwa kuwa klabu haitaki kumuuza.
Wakiwa Thailand, Man United wanatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na Liverpool itakayopigwa Julai 12 na baada ya hapo wataelekea Australia na kucheza mechi dhidi ya timu za Melbourne Victory, Crystal Palace na Aston Villa kabla ya kurudi Manchester Julai 25.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 37, msimu ulioisha aliifungia United mabao 24 na inaaminika kwamba anataka kwenda katika timu ambayo itampa nafasi ya kucheza katika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na tayari klabu za Chelsea na Napoli zimeshaonyesha nia ya kutaka huduma ya mchezaji huyo ambaye ana mwaka mmoja katika mkataba wake Man United.
