Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Simba Queens, Charles Lukula, ameeleza kufurahishwa na kiwango bora cha wachezaji wake hadi kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Aliance Girls.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake uliochezwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, mabao ya Simba Queens yalifungwa na mshambuliaji wao raia wa Kenya, Jentrix Shikangwa.
Lukula, alisema malengo yao ni kuhakikisha wanatetea tena taji la ligi na ndio maana kila mchezo ulio mbele yao wanaupa uzito ili waweze kutimiza mipango yao.
“Tulianza ligi vibaya lakini taratibu tumeanza kukaa sawa, mbio za ubingwa si rahisi unapaswa kushinda kila mchezo kwani timu zimepishana pointi chache hivyo ili ujiweke kwenye mazingira mazuri lazima ushinde.
“Simba Queens ni timu kubwa kila wakati inahitaji kupata ushindi, falsafa yangu ni kucheza kwa nafasi, kufunga njia na kufunga mabao naamini tukiendelea na mwendo huu tunaenda kutwaa taji,” alisema Lukula.
Katika mechi nyingine Yanga Princess na JKT Queens zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Jenerali Samuyo, Dar es Salaam na makocha wa timu zote mbili kudai kuwa ilikuwa mechi ngumu na yenye mipango mingi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sebastian Nkoma alisema kabla ya mechi alifahamu joto la mechi hiyo kutokana na uzoefu wa mabingwa hao wa zamani wa ligi hiyo hivyo hata baada ya matokeo alishukuru kwa timu yake kucheza vizuri licha ya kushindwa kuondoka na pointi tatu.
“JKT wamechukua ubingwa mara kadhaa kabla ya kupokelewa na Simba, hivyo nilifahamu ninakutana na timu yenye uzoefu mkubwa na mimi nakuja na timu mpya, mimi pia nikiwa mpya ndani ya timu, mechi ilikuwa ngumu, tulipambana na mwisho imeisha 0-0,” alisema Nkoma.
Naye kocha wa JKT, Ali Ali alisema: “Tunashukuru tumepata pointi moja, tuliingia kwa kuiheshimu Yanga, wana timu nzuri, wana benchi zuri la ufundi hivyo tukacheza kwa tahadhari, tukapambana na mwisho tumeondoka na pointi moja na kilichotuangusha ni safu ya ushambuliaji sababu tuna wachezaji wengi majeruhi eneo hilo.”
Kwa matokeo hayo, Yanga imesalia nafasi ya nne ya msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14 baada ya kushinda mechi nne, sare mbili na kufungwa mara moja wakati JKT ipo kileleni kwa pointi 17.
JKT hadi sasa imeshinda mechi tano na sare mbili wakati Simba Queens inashika nafasi ya pili kwa pointi 16 sawa na Fountain Gate iliyo nafasi ya tatu.