Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi (pichani) amesema ataonesha soka la ushindani na la kuvutia ili kuwapa raha mashabiki wa Yanga kwenye mechi yao na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini Jumamosi hii.
Yanga itaumana na Kaizer katika mchezo wa kirafiki maalum kwa kilele cha Wiki ya Mwananchi itakayopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 jioni.
Kuelekea mechi hiyo, Gamondi amefafanua kuwa wanaingia wakiwa hawana wakati mzuri kimaandalizi kwani wameanza siku kumi nyuma huku kukiwa na wachezaji takriban wanane ambao wamechelewa kuingia kambini lakini pamoja na yote atahakikisha Yanga wanafurahi.
“Niseme tunacheza na timu kubwa kama Kaizer na kiukweli wamekuja tukiwa ndiyo tumeanza maandalizi, tuna kama siku 10 na baadhi ya wachezaji wamechelewa lakini kwa upande wetu benchi la ufundi tunataka kuwatumia wachezaji wote…
“Wengine watacheza dakika chache, wengine hawatacheza sababu wamekuja majeruhi, hawako fiti ila tutajitahidi kuonesha mashabiki kwa namna gani tunaweza kuwa kwenye ubora hata kwa kujiandaa katika siku hizi chache,” alisema Gamondi.
Alisema anahitaji kuonesha soka safi kuleta furaha katika siku hiyo maalum, wakihitaji ushindi ingawa kushinda au kufungwa kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya kama hizi huwa si kitu zaidi ya kutazama kuijenga timu.
Gamondi alibainisha pia kufahamu jinsi gani kuna presha kuifundisha Yanga, kitu ambacho si kigeni kwake kutokana na utamaduni wa soka ulivyo hata kwenye taifa la Argentina anakotokea.
“Presha inakuwa kubwa pia kutokana na ubora ilioonesha timu msimu uliopita, ilikuwa nzuri mno na nishukuru kila mmoja aliyefanikisha hilo na sasa tunahitaji kufanya zaidi, na mpira hautabiriki na pia naziheshimu timu nyingine za ligi ambazo zitapambana kushinda.
“Japo na sisi tunapambana kutengeneza timu yenye nguvu, timu kubwa ambayo itashindana kwa miaka kujaribu kushinda kila kitu, timu inaposhinda inahitaji kuendelea kubaki hapo na mashabiki wanapenda hivyo,” alisema Gamondi.
Yanga ambayo msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, msimu ujao itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Gamondi amekiri kuwa watakutana na changamoto kubwa lakini watapambana vya kutosha.
Klabu hiyo ilianza shamra za sherehe hizo zinazohitimishwa Jumamosi hii, siku sita zilizopita katika uzinduzi uliofanyika Uwanja wa Furahisha, Mwanza.
Mbali na mechi hiyo pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Billnass, Kassim Mganga, Mzee wa Bwax, Christian Bella, Madee, Sholo Mwamba, Dulla Makabili, Mavokali na wengineo.
Taarifa nyingine pia inafafanua kuwa katika sherehe hizo Yanga imepanga kumuaga aliyekuwa straika wao, Fiston Mayele na yeye pia kuzungumza na mashabiki mara ya mwisho kabla ya kuanza kibarua chake katika klabu aliyotimkia.