Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga kimewasili mjini Lubumbashi, DR Congo jana Alhamisi na kuanza mazoezi ya kujiweka sawa na kupunguza uchovu, tayari kwa kuivaa TP Mazembe.
Yanga iliyoondoka Dar es Salaam jana asubuhi na kutua Lubumbashi baadaye saa 9 alasiri, baada ya mapumziko jana, jioni ilifanya mazoezi.
Meneja wa miamba hiyo, Walter Harison ameeleza kuwa timu hiyo imewasili salama na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa wenyeji wao, Mazembe kitu kilichoongeza matumaini yao ya kushinda mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nashukuru Mungu tumewasili salama, hali ya hewa ni nzuri, wachezaji wetu wote wapo katika hali nzuri na ratiba yetu ni kwamba baada ya mapumziko jioni ya leo tutakwenda kufanya mazoezi mepesi kuweka miili ya wachezaji wetu sawa,” alisema Walter.
Alisema kuwa wachezaji wao ambao walikuwa kwenye timu za mataifa ya nje tofauti na Tanzania wanatarajia kuwapokea kesho Ijumaa wakitokea kwenye nchi zao.
Alisema mpaka sasa benchi lao la ufundi linaloongozwa na kocha Nasreddine Nabi (pichani juu) lipo katika wakati mzuri kupanga mikakati yao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kujiweka katika malengo yao ya kumaliza vinara kwenye kundi hilo.
Alisema lengo lao ni kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo ili kuanzia ugenini mechi yao ya kwanza ya hatua ya robo fainali kitu ambacho anaamini itakuwa ni faida kwao.
Kwa sasa Yanga inashika nafasi ya kwanza kwenye Kundi D ikiwa na pointi 10 sawa na US Monastir lakini endapo itapoteza mchezo dhidi ya Mazembe na Monastir ikashinda mchezo wao dhidi ya Real Bamako, Yanga itashuka hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo.