London, England
Kocha wa Burnley, Vincent Kompany amesema kiwango cha waamuzi wa Ligi Kuu England (EPL) kimeshuka, hoja inayounga mkono shutuma ambazo waamuzi hao wamekuwa wakikutana nazo msimu huu.
Waamuzi wa EPL hususan msimu huu wamejikuta wakibebeshwa lawama za mara kwa mara kutokana na maamuzi ya utata ambayo wamekuwa wakiyatoa katika baadhi ya mechi.
Timu ya Burnley ilibaki na wachezaji 10 uwanjani katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Chelsea na baadaye Kompany kupewa kadi nyekundu kwa kulalamikia penalti iliyoonekana kuwa na utata.
Burnley ambayo inanyemelewa na janga la kushuka daraja, inashika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi hiyo zikiwa zimebaki mechi tisa na katika mechi hiyo na Chelsea kwenye dimba la Stamford Bridge ilitoka sare ya mabao 2-2.
“Hasira zimekuja kutokana na makosa yanayoendelea siku hadi siku na wakati wote yamekuwa yakizua mjadala,” alisema Kompany katika mkutano na waandishi wa habari.
“Madhara yake yanakuwa ni katika pointi na msimu wote, nafikiri mambo yote hayo yanakupa mawazo ya kuwa mwenye hasira lakini yakijitokeza tena nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo ili nikae kimya, nafikiri haitatokea tena msimu huu,” alisema Kompany.
Kompany alisema anaendelea kusema kile anachofikiri, ambacho hawezi kukiacha hivi hivi na analazimika kusema kwamba waamuzi kiwango chao hakijawa kizuri msimu huu na anasema hivyo katika namna ya kujenga.
Kocha huyo ambaye baadaye aliwaomba radhi waamuzi kwa kauli hiyo pia alikumbushia kauli yake ya mwaka jana aliposema kwamba EPL kuna waamuzi bora duniani lakini katika mtazamo wa kawaida tu hali hiyo haioni kwa mwaka huu.