Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba, Zoran Maki ameeleza kufurahishwa kwake na mechi za kirafiki za kimataifa watakazocheza nchini Sudan ambazo zitasaidia kuwajenga zaidi kuelekea kwenye ushindani wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Timu hiyo inatarajia kupaa kuelekea nchini humo Agosti 26, mwaka huu kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya Al-Hilal ya Sudan na Asante Kotoko ya Ghana.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa kocha wa timu hiyo, Zoran Maki amezifurahia mechi hizo kwani zitaendelea kuwajenga kiushindani wachezaji wake hata baada ya kusimama kwa ligi hivi sasa kutokana na mechi za timu za taifa.
Pia akaongeza kuwa mechi hizo ni mahsusi kama kipimo kutokana na kibarua kigumu walichokuwa nacho dhidi ya Nyassa Big Bullets ya Malawi watakayocheza nayo kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tumepata mwaliko kutoka Al-Hilal Sudan kama sisi tulivyoandaa mashindano madogo ya kirafiki ya kimataifa ya Simba Super Cup tukawaalika wao na wao sasa wametualika sisi na kwa kufahamu umuhimu wa jambo hilo tumekubali mwaliko huu.
“Ni kipimo sahihi sana unapokwenda kucheza Ligi ya Mabingwa lazima upate kipimo kutoka kwa watu mbalimbali, timu mbalimbali kutoka Afrika, Hilal ni kipimo sahihi sana unapokwenda kucheza na Nyassa Big Bullets kama ilivyo kwa Kotoko.
“Kwa hiyo kocha mwenyewe binafsi yake ameridhika kwa timu tunazoenda kucheza nazo na anaona kwamba ni kipimo sahihi sana kuelekea kwenye michuano ambayo iko mbele yetu,” alifafanua Ally.
Wekundu hao ambao wameshinda michezo yao yote miwili ya awali ya ligi na kukaa kileleni kwa pointi sita, itaumana na Hilal Agosti 28 kisha itaivaa Kotoko Agosti 31 kabla ya kurejea Dar es Salaam kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya AS Arta ya Djibouti mnamo Septemba 3, mwaka huu.
Kwenye mechi yao dhidi ya AS Atar, Simba pia inatarajia kupata ushindani mkubwa kutokana na timu hiyo kuwa na nyota wengi waliowahi kung’ara Ulaya kama Solomon Kalou aliyewahi kukipiga Chelsea, Alexander Song aliyewika Arsenal kisha Barcelona.
Wengine ni Dany Nounkeu aliyewika na Galatasaray na Granada, pia yumo kipa Carlos Kameni aliyefanya vizuri akiwa na Malaga na Espanyol, Alain Traoré aliyekipiga AS Monaco na FC Lorent na wengine wengi.
