Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG), Lionel Messi juzi Jumapili aliweka rekodi ya kufunga mabao 700 kwenye klabu na jana Jumatatu ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa Fifa.
Katika tuzo hiyo, Messi amembwaga mshambulijai mwenzake wa PSG, Kylian Mbappe pamoja na Karim Benzema wa Real Madrid ambao awali walikuwa wakitajwa kuwa wangeweza kubeba tuzo hiyo.
Messi alifunga bao la 700 katika mechi ya PSG na Marseille iliyoisha kwa PSG kutoka na ushindi wa mabao 3-0 huku moja likifungwa na Messi na mawili yakifungwa na Mbappe.
Mafanikio ya Argentina kubeba Kombe la Dunia Desemba mwaka jana ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kupata mafanikio hayo makubwa katika soka baada ya miaka 36, ndiyo yanayoaminika kumfanya Messi abebe tuzo hiyo ya Fifa.
“Inavutia, ni mwaka mzuri na ni heshima kwangu mimi kuwa hapa usiku huu na kushinda tuzo hii,” alisema Messi ambaye alikuwa amekaa jirani na Mbappe katika hafla ya utoaji tuzo hizo.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Messi kubeba tuzo bora ya Fifa, akifanya hivyo mara ya kwanza mwaka 2019 ingawa nyota huyo wa zamani wa Barcelona pia ana tuzo maarufu za Ballon d’Or saba.
“Napenda kumshukuru sana kocha (Lionel) Scaloni na wachezaji wenzangu bila ya wao nisingeweza kuwa hapa,” alisema Messi akimshukuru Scaloni ambaye ni kocha wa timu ya Taifa ya Argentina.
“Nimefanikisha ndoto, nimekuwa mwenye matumaini kwa muda mrefu na hatimaye nimefanikisha, ni ndoto ya kila mchezaji, ni wachache mno wanaoweza kufanikisha hili, na mimi ni mwenye bahati,” alisema Messi.
Mchezaji wa timu ya wanawake ya Barcelona, Alexia Putellas alishinda tuzo hiyo kwa upande wa wanawake akiwa amefanya hivyo kwa mara ya pili mfululizo.
Naye kocha wa Argentina, Scaloni alishinda tuzo ya kocha bora kwa upande wa wanaume kama ambavyo kipa wa Argentina, Emiliano Martinez alishinda tuzo ya kipa bora kwa wanaume.
Wengine walioondoka na tuzo ni Mary Earps aliyetwaa tuzo ya kipa bora kwa wanawake na Sarin Wiegman, kocha wa England aliyetwaa tuzo ya kocha bora kwa upande wa wanawake.