Manchester, England
Klabu ya soka ya Manchester United imetoa onyo kwa klabu ya Paris Saint-German (PSG) ya Ufaransa ambayo inadaiwa kumnyatia, Marcus Rashford na kudai kuwa mshambulaiji huyo hauzwi.
Man Utd imetoa onyo hilo baada ya kuwapo habari kwamba wakala wa Rashford amekutana na kufanya kikao na vigogo wa PSG jijini Paris wiki iliyopita huku wakidaiwa kujadili uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo.
PSG inadaiwa kuwa katika mpango wa kusajili mshambuliaji wa kuiongezea nguvu safu yao ya ushambuliaji huku Rashford akitajwa kuwa katika rada zao lakini Man Utd baada ya kulibaini hilo inadaiwa kusema kwamba haitokuwa tayari kukaa mezani kujadili kumuuza mchezaji huyo.
Rashford ana mwaka mmoja katika mkataba wake na Man Utd huku klabu hiyo ikiwa na nafasi ya kumuongeza mkataba wa mwaka mwingine mmoja hali ambayo inamfanya mchezaji huyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kubaki Old Trafford hadi mwaka 2024.
Habari za ndani zinadai kwamba PSG imekuwa ikimvizia mshambuliaji huyo tangu mwaka 2021 wakati timu hiyo ikinolewa na kocha Mauricio Pochettino ikidaiwa kuwa tayari kuongeza dau lakini haikuwahi kufanya mawasiliano yoyote na Man Utd kuhusu ada ya uhamisho.
PSG inadaiwa ipo tayari kutoa kitita cha Pauni 60 milioni kwa ajili ya kuinasa saini ya Rashford wakati Man Utd inaamini thamani ya mchezaji huyo inaweza kuwa mara mbili ya pesa ambayo PSG wanaitaja.
Kwa sasa Rashford ni mmoja wa wachezaji muhimu wa kocha Erik ten Hag katika kikosi cha Man Utd ambacho kimeanza msimu wa 2022/23 wa Ligi Kuu England kwa kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Brighton na inaaminika kuwa Ten Hag ana nia ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji hivyo ni wazi hatokuwa tayari kuona Rashford anaondoka.
Kimataifa Man Utd yaionya PSG kuhusu Rashford
Man Utd yaionya PSG kuhusu Rashford
Read also