Manchester, England
Mashabiki Liverpool waliamini ushindi wao wa kwanza Ligi Kuu England ungepatikana katika mechi yao na Man Utd lakini walisahau kwamba licha ya mwanzo mbaya, Man Utd inabaki kuwa timu kubwa, wakajikuta wakilala kwa mabao 2-1 kwenye dimba la Old Trafford.
Matumaini ya mashabiki wa Liverpool yalichangiwa na rekodi mbovu ya Man Utd katika mechi mbili za kwanza za ligi hiyo dhidi ya timu zinazoonekana kuwa ni ndogo, ilipigwa mabao 2-0 na Brighton kisha ikapigwa mabao 4-0 na Brentford lakini Jumatatu ikabadili kila kitu kwa ushindi dhidi ya timu ya kubwa.
Dakika ya 16, Sancho aliitanguliza Man Uted alipoandika bao la kwanza akionyesha uwezo mkubwa wa kutulia na kumiliki mpira, dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili, Rashford akiitumia vizuri pasi ya Anthony Martial aliipatia Man Utd bao la pili.
Juhudi za Liverpool kutaka kubadili matokeo ziliishia kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Mohamed Salah zikiwa zimebakia dakika tisa mpira kumalizika.
Ushindi huo pamoja na mambo mengine inaaminika umechangiwa na uamuzi mgumu wa kocha Erik ten Hag kuwaweka benchi nahodha Harry Maguire na mkongwe Cristiano Ronaldo na hatimaye kikosi chake kikaonyesha ukomavu ambao umetosha kuibua matumaini mapya ya zama mpya kwa timu hiyo, matumaini ambayo yalipotea miongoni mwa mashabiki wake.
Kwa bao lake Rashford sasa anakuwa amefikisha mabao matano aliyofunga katika mechi dhidi ya Liverpool akiwa amezidiwa na Wayne Rooney mwenye mabao sita lakini jambo la kufurahisha kwa Rashford ni kwamba Rooney kabla ya mechi hiyo alimshauri Ten Hag asimpange Rashford na Ronaldo lakini Ten Hag alimpanga na kumuweka benchi Ronaldo hadi alipompa nafasi dakika nne kabla ya mpira kumalizika akiingia badala ya Rashford.
Rooney alisema kwamba Ten Hag anahitaji kutumia damu changa na kumtolea mfano Rashford ambaye hakuifungia timu hiyo bao tangu Januari lakini sasa ni wazi amefuta ukame huo huenda mambo mazuri yakaanza kuonekana kwa mchezaji huyo.
Liverpool ambayo imeanza ligi kwa sare mbili, sasa inakuwa imepoteza mechi ya 29 dhidi ya Man Utd katika Ligi Kuu England, ikiwa ni mechi nane zaidi walizopoteza kuliko mechi zao na timu nyingine yoyote katika historia ya ligi hiyo.
Kwa upande wa Man Utd ambayo msimu uliopita ilinyanyaswa na Liverpool, ushindi wao wa jana mbali na kuwapa pointi tatu muhimu, pia huenda ukapunguza hasira za mashabiki wa timu hiyo ambao kabla ya mechi hiyo waliandamana kwa maelfu wakionyesha hasira zao dhidi ya mmiliki wa klabu hiyo, Familia ya Glazer.
Mashabiki hao wakiwa na mabango yaliyokuwa yakimpigia debe bilionea wa London, Sir Jim Ratcliffe wakitaka apewe fursa ya kununua hisa nyingi katika klabu hiyo.
Mei mwaka jana mechi ya Man Utd na Liverpool kwenye dimba la Old Trafford ililazimika kuahirishwa kwa sababu ya maandamano ya mashabiki.
Matokeo ya mechi nyingine za wikiendi ni kama ifuatavyo
Leeds 3-0 Chelsea
West Han 0-2 Brighton
Newcastle 3-3 Man City
Tottenham 1-0 Wolverhampton
Crystal Palace 3-1 Aston Villa
Everton 1-1 Nottingham Forest
Fulham 3-2 Brentford
Leicester 1-2 Southampton
Bournemouth 0-3 Arsenal
