Na Hassan Kingu, Dar es Salaam
Yanga leo Jumamosi imeuanza kibabe mzunguko wa pili wa Ligi Kuu NBC kwa kuichapa mabao 3-0 Polisi Tanzania, timu inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera.
Ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 41 katika mechi 16 ikiwa imepoteza mchezo mmoja tu hadi sasa.
Katika mechi ya leo, Polisi awali walionekana kuwa makini wakijihami bila kubabaika kama vile walikuwa wakicheza na timu ya kawaida na si Yanga hali iliyoibua matumaini kwamba huenda Zahera alitumia uzoefu wake na kwa jinsi anavyoijua Yanga kuja na maajabu na haikushangaza hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hakuna timu iliyopata bao huku Polisi wakionyesha uwezo.
Yanga hata hivyo ilianza kuhesabu bao lake la kwanza dakika mbili baada ya mapumziko mfungaji akiwa ni Jesus Moloko aliyeitumia vizuri pasi ya Benard Morrison ambaye aliingia uwanjani akitokea benchi na kutoa pasi ya bao.
Fiston Mayele aliendelea kuimarisha rekodi yake ya mabao katika ligi baada ya kuifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 77 na hivyo kufikisha jumla ya mabao 11 akiwa ndiye kinara wa mabao akimuacha Moses Phiri wa Simba ambaye awali wote walifungana wakiwa na mabao 10.
Clement Mzize, mshambuliaji anayeibukia Yanga ndiye aliyekamilisha rekodi ya mabao ya Yanga baada ya kuandika bao la tatu dakika nne kabla ya mpira kumalizika.
Huu unakuwa ushindi wa pili kwa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Ligi Kuu NBC msimu huu, katika mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, Yanga ilitoka na ushindi wa mabao 2-1.
Soka Yanga yaanza kibabe mzunguko wa pili
Yanga yaanza kibabe mzunguko wa pili
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
