Riyadh, Saudi Arabia
Mbarazil, VinÃcius Júnior ameibuka shujaa baada ya kufunga mabao matatu (hat-trick) wakati Real Madrid ikiwanyuka mahasimu wao, Barcelona mabao 4-1 na kutawazwa vinara wa Super Cup Hispania.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jana Jumapili mjini Riyadh, Real wakiongozwa vyema na mastaa wake watatu, Jude Bellingham, Rodrygo na Vinicius walikuwa wasumbufu kwa safu ya ulinzi ya Barca.
Haikushangaza kwa timu hiyo kupata bao la kuongoza dakika ya saba, bao ambalo Vinicius alilifunga akiitumia pasi ya Bellingham ambaye akiwa amezungukwa na wachezaji watatu wa Barca aliwazidi ujanja na kutoa pasi iliyozaa bao hilo.
Vinicius aliongeza bao la pili dakika tatu baadaye kabla ya Barca kupata bao pekee dakika ya 33 lililofungwa na Robert Lewandowski na Vinicius akaongeza bao la tatu dakika ya 39 lililozifanya timu kwenda mapumziko, Real ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Dakika 20 baada ya kuanza kipindi cha pili, Real walikamilisha karamu ya mabao kwa kuandika bao la nne lililofungwa kwa penalti na Rodrygo, penalti iliyotolewa baada ya beki wa Barca, Ronald Araujo kumchezea rafu Vinicius.
Barca walipata pigo dakika ya 71 na kujikuta wakibaki 10 uwanjani baada ya beki wao, Ronald Araujo kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Vinicius mara mbili.
“Sikutarajia tungeweza kufunga mabao matatu kwa haraka, lakini tulifaidika na namna safu yao ya ulinzi ilivyokuwa tukiwa na Vinicius aliyejaa hamasa,” alisema kocha wa Real, Carlo Ancelotti.
Ancelotti pia alisema kwamba mechi ilikuwa ngumu lakini matokeo yamekuwa makubwa mno kwa Barca kwa namna walivyocheza, wakati matokeo yakiwa 3-1 timu zilikuwa nguvu sawa lakini ilipokuwa 4-1 Barca kidogo wakalegea.
Matokeo hayo yanazidi kumuweka katika wakati mgumu kocha wa Barca, Xavi ambaye amekuwa akilaumiwa na mashabiki na baadhi ya vyombo vya habari kutokana na mwenendo usiovutia wa timu hiyo.
“Hatujaonesha kiwango kilichotakiwa kwa mechi ya aina hii, tulicheza mechi hovyo, hatukuwa salama, Madrid walituadhibu kwa mashambulizi ya kushtukiza, naomba msamaha kwa mashabiki kwa sababu ilikuwa ngumu kwetu kupambana na tumeonesha kuwa kikosi cha hovyo,” alisema Xavi.
Barca inashika nafasi ya sita kwenye La Liga ikiwa na pointi 41, pointi nane nyuma ya vinara Girona na saba nyuma ya mahasimu wao Real wanaoshika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo maarufu duniani.