Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior na Rais wa umoja wa Ligi Kuu Hispania au La Liga, Javier Tebas wameingia katika mzozo wakipingana msimamo kuhusu kukabiliana na vitendo vya ubaguzi wa rangi kwenye viwanja vya soka.
Hivi karibuni, Vinicius ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Brazil, aliendelea kuwashutuhumu La Liga kwa kutofanya chochote kwa mashabiki wenye hulka za ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji baada ya video za mashabiki kuonekana kwenye mitandao ya kijamii wakitamka maneno ya kibaguzi na kumrushia vitu mbalimbali mchezaji huyo akiwa uwanjani.
La Liga walitoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakishutumu matukio yote ya kibaguzi na kauli za aina hiyo na kuongeza kwamba wanafuatilia matukio ya ubaguzi wa rangi yanayojitokeza kwenye viwanja vya soka.
Vinicius alijikuta akiwa mlengwa wa matukio ya ubaguzi kwenye Uwanja wa Jose Zorrilla wakati akitoka uwanjani baada ya kufanyika mabadiliko katika mechi dhidi ya Valladolid, mechi ambayo Real Madrid walishinda kwa mabao 2-0.
“Ubaguzi wa rangi unaendelea kwenye viwanja vya soka na unashuhudiwa kwenye klabu kubwa duniani na La Liga wanaendelea kuwa vile vile, hakuna wanachofanya,” alisema Vinicius kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
“Nitaendelea nikiwa kichwa mbele kushangilia ushindi wangu na ule wa Madrid,” aliongeza Vinicius kauli ambayo ilimuibua Tebas ambaye naye alimpinga akitumia mitandao ya kijamii.
“Katika La Liga tumekuwa tukipambana na vitendo vya ubaguzi wa rangi kwa miaka mingi, @Vinicius Junior si haki na si kweli kusema kwamba La Liga haifanyi lolote dhidi ya ubaguzi wa rangi, jielimishe. Tuko kwa ajili yako ili kwa pamoja twende katika muelekeo mmoja,” alisema Tebas.
Tebas pia alitoa taarifa rasmi inayoeleza kwamba La Liga wanafuatilia kwa karibu tukio alilofanyiwa Vinicius katika mechi hiyo.
Hii si mara ya kwanza kwa Vinicius mwenye umri wa miaka 22 kukumbana na adha ya ubaguzi wa rangi, Septemba mwaka jana mashabiki wanaoaminika kuwa wa Atletico Madrid walionekana kwenye picha za video wakimdhihaki mchezaji huyo kwa maneno na ishara za kibaguzi nje ya Uwanja wa Wanda Metropolitan muda mfupi kabla ya mechi dhidi ya Real Madrid.
