Na mwandishi wetu
Klabu ya Singida Fountain Gate leo Ijumaa imeeleza kuwa kuelekea msimu ujao wataweka kambi yao mkoani Arusha na si nchini Tunisia kama walivyotangaza hapo awali.
Singida imefafanua kuwa ufinyu wa muda na kuchelewa kukamilika kwa usajili wa wachezaji imekuwa kikwazo cha safari yao ya Tunisia ambako walieleza walipewa mwaliko maalum na klabu ya US Monastir ya nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao kijamii, timu hiyo inatarajia kuanza kambi yake rasmi Julai 10, mwaka huu kabla ya baadae kutoa ufafanuzi wa ratiba nzima ya kambi hiyo.
“Awali maandalizi yalikuwa yafanyikie kwenye nchi ya Tunisia lakini kutokana na ufinyu wa muda na kuchelewa kukamilika kwa zoezi la usajili wa wachezaji, tumelazimika kubaki nchini ili wachezaji wote waweze kushiriki maandalizi haya kwa wakati.
“Taarifa zaidi kuhusu kambi yetu ya Arusha na maandalizi kwa ujumla zitaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari na kurasa zetu za mitandao ya kijamii,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mpaka sasa Singida haijatangaza usajili wowote ilioufanya zaidi ya kuwaongezea mkataba baadhi ya wachezaji wake muhimu huku pia ikihusishwa na baadhi ya wachezaji wa kimataifa.
Singida FG msimu ujao wa 2023-24 mbali na Ligi Kuu ya NBC na michuano mingine ya ndani, timu hiyo pia itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Soka Singida FG sasa kuweka kambi Arusha
Singida FG sasa kuweka kambi Arusha
Read also
