Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Kemnedy Musonda (pichani) na kiungo Clatous Chama wa Simba wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ kinachoundwa na wachezaji 27.
Kocha Mkuu wa Zambia, Avram Grant amewataja wachezaji hao kuelekea mechi zao mbili dhidi ya Lessotho za kufuzu fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2023) zinazotarajia kufanyika nchini Ivory Coast.
Katika kikosi hicho, Grant pia amemjumuisha Kambole, mshambuliaji wa Yanga anayekipiga kwa mkopo Zesco United ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoitwa mara ya mwisho katika kikosi hicho Novemba, 2019.
Kambole aliacha kuitwa Chipolopolo wakati amejiunga na Kazier Chief ya Afrika Kusini alikodumu kwa misimu mitatu kabla ya kutimkia Yanga mwanzoni mwa msimu huu.
Pia, Grant aliyewahi kuinoa Chelsea amemjumuisha kiungo wa zamani wa Simba, Larry Bwalya anayekipiga Amazulu ya Afrika Kusini akiungana na nyota wengine, Patson Daka (Leicester City, England), Kings Kangwa (Red Star Belgrade, Serbia), Emmanuel Banda (Djurgarden, Sweden), Aime Mabika (Inter-Miami, USA) na wengine.
Zambia itaumana na Lesotho Machi 23 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Machi 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Dobsonville, Johannesburg.
Kimataifa Musonda, Chama waitwa Chipolopolo
Musonda, Chama waitwa Chipolopolo
Related posts
Read also