Barcelona, Hispania
Barca imedhamiria kumrudisha straika wake wa zamani, Lionel Messi baada ya rais wa klabu hiyo, Joan Laporta kusema wanaweza kushindana na ofa za Saudi Arabia licha ya matatizo yao ya kifedha.
Baada ya msimu huu Messi ataihama klabu yake ya sasa ya PSG ya Ufaransa akiwa kamaliza mkataba huku kukiwa na habari kwamba ana ofa nono Saudi Arabia katika klabu ya Al Hilal.
Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya Argentina ambaye aliiwezesha taji la Dunia, Desemba mwaka jana, mwezi ujao atatimiza miaka 36 na Barca wanaamini ni wakati sahihi mchezaji huyo kurejeshwa ili astaafie katika klabu hiyo aliyoanza kuichezea kwenye akademi yao.
“Tunawaheshimu Saudi Arabia, kuna kazi kubwa nzuri na uwekezaji unaoendelea katika ligi ya huko, lakini Barca itabaki kuwa Barca,” alisema Laporta.
“Barca ni nyumbani kwake, Barca inaweza kushindana na yeyote, historia ya klabu hii na hisia za mashabiki wetu 400 milioni tuko imara sana,” alisema Laporta.
Hali ya kiuchumi ya Barca ni kikwazo kushindana katika kuisaka saini ya Messi kwa kile ambacho Messi anaweza kupewa Saudi Arabia lakini wanaamini mabosi wa La Liga wanaosimamia sheria kali za usajili watawaruhusu kufanya usajili katika msimu wa majira ya kiangazi.
“Klabu inapitia kipindi kigumu katika mipango ya kifedha lakini tunafanya juhudi kutengeneza timu ya ushindani kwa ajili ya msimu ujao, tunasubiri kama La Liga watapitisha mpango wetu wa matumizi,” alisema Laporta.
Ugumu mwingine wa Messi kurudi Barca, klabu ambayo ameifungia mabao 672 katika mechi 778 ni uhusiano wake na Laporta ambao uliyumba mwaka 2021 na kujikuta akihamia PSG.
Laporta hata hivyo alizungumzia suala hilo akisema kwamba amekuwa akifanya mazungumzo na mchezaji huyo na wameshayamaliza.
“Nimezungumza naye katika siku za karibuni ili kuweka mambo sawa baada ya mimi kuweka mbele maslahi ya klabu kuliko chochote akiwamo Messi, mchezaji bora duniani, yalikuwa mazungumzo mazuri, tumerudisha uhusiano tuliokuwa nao miaka mingi,” alisema Laporta.
Laporta pia alisema kwamba halikuwa jambo zuri kumuona Messi akizomewa na mashabiki wa PSG baada ya kusimamishwa kwa kosa la kwenda Saudi Arabia bila ruhusa kwa masuala ya kibiashara.
