London, England
Liverpool iliyotoka kuifunga Man United mabao 7-0, imelala kwa bao 1-0 mbele ya Bournemouth, timu ambayo Liverpool iliweka rekodi ya kuichapa mabao 9-0 timu hizo zilipokutana mara ya mwisho.
Ushindi huo wa nyumbani kwa Bournemouth unakuwa kitu muhimu kwa timu hiyo ambayo kwa sasa inapambana kwa hali na mali ili kujinasua na janga la kushuka daraja linaloinyemelea.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyochezwa jana Jumamosi, Mohamed Salah, mfungaji bora wa msimu uliopita, ndiye aliyekosa penalti wakati Liverpool ikipoteza pointi tatu muhimu.
Salah ambaye hivi karibuni amevunja rekodi na kuwa mfungaji wa wakati wote wa Liverpool mwenye mabao mengi (mabao 129) katika Ligi Kuu England, alikosa penalti iliyotolewa dakika ya 68 baada ya Adam Smith kuunawa mpira wa kichwa uliopigwa na Diogo Jota.
Bao hilo pekee la Bournemouth lilifungwa na Philip Billing katika dakika ya 28 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Dango Ouattara. Hilo ni bao la sita kwa Billing katika Ligi Kuu England msimu huu.
Matokeo ya mchezo huo yamesaidia kuitoa Bournemouth kwenye janga la kushuka daraja ikiwa imefikisha pointi 24 na kuchupa hadi nafasi ya 17 kutoka nafasi ya 20 iliyokuwa awali.
Bournemouth sasa inasubiri matokeo ya mechi za Southampton dhidi ya Man United na West Ham dhidi ya Aston Villa zinazochezwa jioni ya leo Jumapili ambazo zinaweza kubadili msimamo wa ligi.
Kwa Liverpool matokeo hayo yameathiri mbio za timu hiyo kusaka tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, inabaki nafasi ya tano na imeachwa na Tottenham inayoshika nafasi ya nne kwa tofauti ya pointi sita.
Ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Man United ulionekana ungekuwa chachu kwa timu hiyo kuendelea kutoa vipigo katika Ligi Kuu England lakini timu inayotajwa kuwa dhaifu ya Bournemouth imebadili mtazamo huo.
Matokeo ya mechi hiyo yameacha swali kama Liverpool itarudi katika ubora ulioanza kuonekana katika mechi yake na Man United au itarudi katika kusuasua baada ya matokeo ya mechi na Bournemouth?
Matokeo ya mechi za Jumamosi Ligi Kuu England ni kama ifuatavyo…
Bournemouth 1-0 Liverpool
Everton 1-0 Brentford
Leeds 2-2 Brighton
Leicester 1-3 Chelsea
Tottenham 3-1 Nottm Forest
Crystal Palace 0-1 Man City
Kimataifa Liverpool yatikiswa England
Liverpool yatikiswa England
Read also