Na mwandishi wetu Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki michuano mikubwa mitatu ya klabu Ulaya inayosimamiwa na Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa). Hiyo ni baada ya timu yake ya PAOK FC ya Ugiriki kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Europa Conference League kwa kuifumua Hearts ya Scotland jumla ya mabao 6-1. Kwenye mchezo wa ugenini PAOK ilishinda mabao 2-1 kabla ya jana kushinda mabao 4-0. Samatta aliyetua PAOK msimu huu alishashiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2019-20 akiwa na Genk ya Ubelgiji, ikipangwa Kundi E dhidi ya timu za Liverpool, Napoli na RB Salzburg. Katika kundi hilo, Genk ilimaliza mkiani ikiwa na pointi moja lakini Samatta alifunga mabao matatu katika hatua hiyo. Samatta pia ameshiriki Europa League mara tatu akiwa na timu mbili tofauti. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2016-17 akiwa Genk na kutolewa robo fainali kabla ya kuishia hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo msimu wa 2018-19. Msimu wa 2021-22 akiwa na Royal Antwerp waliishia kwenye makundi. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC na TP Mazembe ya DR Congo katika misimu mitatu aliyoshiriki Europa League alifanikiwa kufunga mabao manane katika mechi 25 alizocheza. Europa Conference Ligi ni michuano mipya ya klabu barani Ulaya iliyoanzishwa takriban misimu miwili iliyopita, ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Ligi ya Mabingwa na Europa Ligi.
Kimataifa Samatta aweka rekodi Ulaya
Samatta aweka rekodi Ulaya
Read also