Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na Mohamed Hussein ‘Zimbee Jr’ na Tarryn Allarakhia huku akioneshwa kukerwa na wachezaji wasiojituma.
Amrouche alisema hayo baada ya kikosi chake kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Misri kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja Cairo, Misri.
Amrouche alisema lazima wakubaliane na uhalisia sababu kuna baadhi ya wachezaji walicheza chini ya kiwango alichotegemea katika mchezo huo maalum wa kujiandaa na michuano ya Afcon itakayoanza kuunguruma Januari 13, mwaka huu.
“Kuna wachezaji walichokitoa si kile nilichotarajia, hawafanani na majina yao, tunahitaji wachezaji ambao wanaweza kufanya kitu kwa ajili ya timu, nimefurahishwa na baadhi ya wachezaji lakini pia sijafurahishwa na wengine na hatuna muda wa kutosha kurekebisha yote.
“Nimefurahishwa na urejeo wa Mohamed Hussein lakini pia nimefurahishwa na Taryn, ni wachezaji ambao wamekidhi, kama sijafurahishwa zaidi naweza kuwarudisha nyumbani huo ndio ukweli,” alisema Amrouche.
Naye Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alisema mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Misri ni kipimo tosha kwao kabla ya kwenda kuwavaa Morocco kwenye mechi ya kwanza ya fainali ya mataifa ya Afrika, Januari 17.
“Misri ni timu nzuri na kipimo kizuri kwa Taifa Stars nadhani mwalimu atakuwa ameona ni maeneo gani anatakiwa afanyie marekebisho, na maeneo gani tulikuwa wazuri,” alisema Samatta.