Nairobi, Kenya
Ikiwa na wachezaji 10 uwanjani, timu ya taifa ya Kenya, imelazimisha sare ya bao 1-1 na Angola katika mechi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Timu hiyo maarufu Harambee Stars ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kasarani, Alhamisi Agosti 7, 2025, ilianza kutikiswa nyavu zake dakika ya saba kwa bao lililofungwa na Joao Paciencia.
Dakika tano baadaye juhudi za Harambee zilizaa matunda baada ya timu hiyo kupata bao la penalti lililofungwa na kiungo Austine Odhiambo aliyemchambua vyema kipa wa Angola, Adilson da Cruz.
Pernalti hiyo ilitolewa na mwamuzi, Sadou Ali Brahamou baada ya Odhiambo ambaye pia ni kiungo wa Gor Mahia, kuchezewa rafu katika eneo la penalti na mwamuzi kujiridhisha kwa kutumia VAR.
Baada ya bao la kusawazisha Harambee walipata pigo dakika ya 21 kwa nyota wao, Marvin Omondi kupewa kadi nyekundu na kuifanya timu hiyo ibaki na wachezaji 10 kwa dakika zilizobaki.
Omondi alipewa kadi hiyo kwa kucheza rafu, awali mwamuzi alimuonesha kadi ya njano lakini baada ya kutumia VAR alibadili maamuzi na kumpa mchezaji huyo kadi nyekundu.
Angola walitumia upungufu wa wachezaji wa Harambee kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara ambayo hata hivyo yalikutana na kikwazo baada ya wachezaji wa Harambee kucheza kwa kujihami zaidi na kushambulia mara chache.
Katika dakika za nyongeza Angola walipata bao lililofungwa kwa kichwa na Kaporal lakini mwamuzi baada ya kufanya marejeo kwenye VAR alikataa bao hilo kwa madai mfungaji aliotea.
Kwa sare hiyo, Harambee ambayo ipo Kundi A imefikisha pointi nne huku wachezaji wake wakiwa na uhakika wa kupata zawadi ya Sh 500,000 za Kenya (Sh 9.5 milioni za Tanzania) kwa kila mmoja ambayo ni ahadi ya Rais wa Kenya, William Ruto.
Kimataifa Harambee yalazimisha sare kwa Angola
Harambee yalazimisha sare kwa Angola
Read also
