Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema timu yake itaingia na mbinu mbadala ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya ikiwamo kuiheshimu timu hiyo ili wapate matokeo.
Simba inatarajia kuikaribisha Horoya ya Guinea katika mchezo wa tano wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo Simba inahitaji ushindi ili ifuzu hatua ya robo fainali baada ya kushinda na kufungwa mechi mbili kwenye michezo ya awali ya Kundi C ya michuano hiyo na kuvuna pointi sita ikiwa nafasi ya pili.
Msimamo wa kundi hilo mpaka sasa unaonesha kinara ni Raja Casablanca aliyekwishafuzu baada ya kushinda michezo minne na kufikisha pointi 12 ingawa ana michezo miwili mkononi.
Simba ikiibuka kidedea katika mchezo dhidi ya Horoya, itafikisha pointi tisa ambazo wengine kwa maana ya Horoya yenye pointi nne na Vipers yenye pointi moja hawawezi kuzifikia.
Mbali na ushindi lakini Simba itaingia dimbani ikitaka kulipiza kisasi pia cha kufungwa bao 1-0 na Horoya ilipokuwa ugenini hasa ikikumbukwa namna Simba ilivyomiliki mchezo lakini ilikosa matokeo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oliveira ambaye hakufafanua kwa undani kuhusu mbinu mbadala badala yake alisisitiza kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu.
“Mchezo hautakuwa rahisi lakini tutaingia kwa lengo moja la kushinda na kuingia robo fainali na kwa hilo tumefanya maandalizi ya kutosha bila kujali ukubwa wa wachezaji tunaokwenda kukutana nao kwa sababu tumeandaa vijana vyema,” alisema Robertinho.
Kocha wa Horoya, Sekou Diego alisema wao pia wamejiandaa vizuri kimbinu kulingana na wapinzani wao na wamekuja Tanzania ili kupata ushindi na kuendelea na safari yao ya kutinga robo fainali.