Doha, Qatar
Shirikisho la Soka Morocco (FMRF) limewasilisha malalamiko Fifa dhidi ya mwamuzi aliyechezesha mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa wakidai aliwanyima penalti.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumatano, Morocco ililala kwa mabao 2-0 lakini timu hiyo ambayo imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia, sasa imemgeuzia kibao mwamuzi wa mechi hiyo, Cesar Ramos kutoka Mexico.
Katika malalamiko yao Morocco wanadai kwamba mwamuzi huyo alitakiwa kuwapa penalti baada ya Theo Hernandez kumchezea rafu Sofiane Boufal lakini hakufanya chochote badala yake alimpa kadi, Boufal kwa madai ya kucheza rafu. Morocco katika mechi hiyo ilizamishwa kwa mabao ya Hernandez na Randal Kolo Muani.
“FMRF imeandika barua Fifa ili kupitia upya maamuzi ya mwamuzi huyo ambayo yaliinyima Morocco penalti mbili za wazi pamoja na matukio mengine,” ilieleza taarifa hiyo. “FMRF sambamba na hilo pia imeshangazwa na kitendo cha VAR kutotumika katika matukio hayo.”
Hoja ya Morocco kutaka kupewa penalti pia iliungwa mkono na baadhi ya wachambuzi mmoja wao akiwa ni mshambuliaji wa zamani wa England, Chris Sutton. “Kwangu mimi naona kama ilikuwa penalti ya Morocco, VAR haifanyi kazi?” alihoji Sutton.
Mwingine aliyekuwa na mawazo kama hayo ni beki wa zamani wa England, Rio Ferdinand, “Nadhani ni penalti kwa rafu ya Sofiane Boufal na si tu kuchezewa rafu.” Morocco au Atlas Lion, kesho Jumamosi itacheza mechi ya kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Croatia.
Kimataifa Morocco yamshushia lawama mwamuzi
Morocco yamshushia lawama mwamuzi
Related posts
Read also
