Riyadh, Saudi Arabia
Kocha Herve Renard amefutwa kazi katika timu ya taifa ya Saudi Arabia, ikiwa ni miezi miwili kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Herve, 57, kocha kutoka Ufaransa amefutwa kazi rasmi Ijumaa Aprili 17, 2026, baada ya kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo maarufu Green Falcons kwa mara ya pili mwaka 2024.
Kabla ya hapo kocha huyo alikuwa na timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar na kuweka historia kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Argentina ambao baadaye waliibuka mabingwa wa dunia.
Baada ya fainali za Kombe la Dunia 2022, Herve aliondoka Saudi Arabia na kujiunga na timu ya taifa ya wanawake Ufaransa ambayo aliiongoza kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 kabla ya kurudi Saudi Arabia kwa mara ya pili.
Kabla ya kutimuliwa kwa Herve, chanzo kimoja cha habari kiliripoti kuwa Saudi Arabia ilikuwa na mpango wa kumuajiri Matt Crocker katika nafasi ya ukurugenzi wa soka kazi ambayo pia amekuwa akifanya katika Shirikisho la Soka Marekani.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazoanza Juni 11, Saudi Arabia imepangwa Kundi H pamoja na timu za Hispania, Cape Verde na Uruguay na mechi yao ya kwanza itakuwa Juni 15 dhidi ya Uruguay.
Kimataifa Kocha Herve afutwa kazi Saudi Arabia
Kocha Herve afutwa kazi Saudi Arabia
Related posts
Read also
