London, England
Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Richarlison (pichani) amesema kwamba kocha wa zamani wa timu hiyo, Antonio Conte alimkaripia kwa takriban saa mbili wakati wakiwa kwenye kikao cha timu hiyo.
Richarlison ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Brazil alikuwa na wakati mgumu kwenye kikosi cha Spurs msimu uliopita wa 2022-23 chini ya Conte kabla ya kocha huyo kutimuliwa mwezi Machi.
Utata baina ya Richarlison na Conte ulianza baada ya mchezaji huyo kumshushia lawama kocha huyo baada ya Spurs kutolewa katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo baadaye Conte alisema kwamba mchezaji huyo ni mbinafsi.
Richarlison hata hivyo alikiri kwamba alikosea kumlaumu kocha wake hadharani na kujikuta akipewa adhabu mbele ya wachezaji wenzake.
“Ni kweli nilifanya upuuzi mimi mwenyewe kwa kusema katika mahojiano baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa lakini baadaye nilimuomba radhi,” alisema Richarlison.
“Nilifikia hatua ya kumwambia kwamba hata kama anataka kuniadhibu anaweza kufanya hivyo, tulimaliza lile pale,” alisema.
“Lakini alitaka pia aoneshe ukali wake mbele ya wachezaji, ni kama kusema kwamba yupo imara na ndiye kiongozi, hiyo ndiyo namna yake ya kukabiliana na watu, na kundi la wachezaji na alitumia kama saa mbili kunishambulia mimi tu kwenye kikao mbele ya kila mtu,” alisema Richarlison.
Richarlison alisema kwamba baada ya tukio lile baadhi ya wachezaji walimwambia asifanye tena alichokifanya na kila mmoja alitaka kuondoka.
Conte alimsajili Richarlison kutoka Everton mwanzoni mwa msimu wa 2022-23 lakini mchezaji huyo alipitia kipindi kigumu kidogo, hakuwa katika kiwango chake bora baada ya kuandamwa na majeraha hadi kuishia kufunga bao moja tu katika Ligi Kuu England.
Richarlison, 26, hata hivyo alisema kwamba baada ya Conte kutimuliwa Spurs aliwasiliana naye na kumuomba radhi. “Nilimtumia ujumbe wa kumuomba radhi kwa sababu ni mtu ambaye aliniajiri na sikumsaidia kwa kiwango alichofikiria, jambo pekee nililoona linafaa kulifanya ni kumuomba radhi.”
Kimataifa Richarlison: Conte alinifokea kwa saa mbili
Richarlison: Conte alinifokea kwa saa mbili
Read also