Na mwandishi wetu
Uongozi wa Azam FC umebainisha kuwa beki wa kulia, Djuma Shabani yupo kwenye timu yao kwa ajili ya kufanya mazoezi tu na hawajamsajili kama inavyoelezwa.
Djuma raia wa DR Congo juzi alionekana akiichezea Azam katika mechi ya kirafiki waliyoshinda mabao 2-1 dhidi ya Arta Solar na hivyo kuwa kama uthibitisho wa kilichokuwa kikidaiwa hivi karibuni kuwa Azam walikuwa wakiisaka saini ya mchezaji huyo aliyekuwa Yanga.
Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabiti (pichani) ameiambia GreenSports leo Jumanne kuwa Djuma amehitaji kufanya nao mazoezi kipindi hiki akiwa mchezaji huru lakini hawajamsajili kwa kuwa tayari timu hiyo imetimiza idadi ya wachezaji 12 wa kigeni.
“Idadi ya wachezaji wa kigeni imeshatimia kwetu, hatuwezi kuongeza mwingine, Djuma amekuja akiwa na barua inayoonesha ni mchezaji huru na anahitaji kufanya mazoezi na timu, hicho ndicho kilichopo hivyo akiona inatosha kufanya mazoezi ni yeye anavyoona zaidi,” alisema Thabiti.
Azam imefanikiwa kumnasa kiungo mkabaji kutoka Yanga, Yanick Bangala lakini pia ilielezwa kuhitaji saini ya Djuma kabla ya suala lake kuchukua muda kumalizika Yanga na hivyo kuchelewa kukamilisha usajili wake mpaka dirisha linafungwa Agosti 31, mwaka huu.
Awali, iliripotiwa kuwa Azam inaweza kumuacha kipa wao, Mcomoro, Ali Ahamada ili Djuma apate nafasi lakini sasa inaweza kusubiriwa mpaka dirisha dogo litakapofunguliwa ndipo yafanyike maamuzi mengine juu ya usajili wa Djuma.