London, England
Kocha wa Tottenham Hostpur, Antonio Conte amejivua lawama akisema si sahihi kulaumiwa peke yake kwa matokeo mabaya ya timu hiyo badala yake ametaka watu wengine katika klabu nao waangaliwe katika jambo hilo.
Jumapili iliyopita timu hiyo ilichapwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa London, Arsenal katika mechi ya Ligi Kuu England na kuifanya timu ipoteze jumla ya mechi tano kati ya tisa za ligi hali inayomuweka pagumu kocha huyo ambaye kesho Alhamisi ana mtihani mwingine mgumu dhidi ya Man City.
“Kwa England nadhani kumekuwa na hulka mbaya, ni kocha tu anayetakiwa kuzungumza na kujieleza,” alisema Conte.
“Sijawahi kuona madaktari wa timu wakija kujieleza, sijawahi kuona klabu au mkurugenzi wa michezo akija hapa kueleza mipango au dira ya klabu, nchini Italia kabla ya kila mechi kuna mtu kutoka katika klabu anayekwenda kuzungumzia mazingira ambayo anayaona kuwa sahihi kwa klabu,” alisema Conte.
“Nafikiri kwa upande wetu pia itakuwa bora, vinginevyo kunakuwa na sura moja tu ya kutoa ufafanuzi kuhusu hali ya klabu ambayo nadhani ingekuwa vizuri kama angetoka mtu katika klabu kuielezea,” alisema kocha huyo Mtaliano akitaka uongozi wa klabu uwepo kwenye mkutano na wanahabari.
Tottenham au Spurs kwa sasa mambo yake si mazuri kwenye Ligi Kuu England ikiwa katika nafasi ya tano ikiachwa na Newcastle inayoshika nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi tano kama ilivyo kwa Man United inayoshika nafasi ya nne.
Conte amejikuta akiwa ‘mhanga mkuu’ wa mwenendo usioridhisha wa Spurs na sasa ameamua kujivua lawama akitaka wabebeshwe lawama hizo na watu wengine kwenye klabu ambao ametaka wawe na nafasi ya kuizungumzia klabu si kila wiki bali japo mara moja kwa mwezi au kila baada ya siku 15.