Algers, Algeria
Yanga imeanza na mguu mbaya mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria katika mechi iliyopigwa Ijumaa hii usiku.
Wenyeji CR Belouizdad wakishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao walioupamba uwanja na jezi nyekundu waliandika bao la kwanza dakika ya 11 lililofungwa na Abdulrahuf Benquit aliyeinasa krosi iliyowababatiza mabeki wa Yanga kabla ya kumkuta mfungaji.
Belouizdad waliongeza bao la pili muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Abdulrahman Meziane aliyeinasa pasi ya chinichini iliyotokea upande wa kushoto kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa wa Yanga, Metacha Mnata.
Bao la ushindi la CR Belouizdad lilifungwa katika dakika nne za nyongeza mfungaji akiwa Lamine Jalow aaliyeunasa mpira ulioanzia kwa Bakir aliyempasia Meziane ambaye alimuunganishia mfungaji wa bao hilo.
Yanga kwa muda wote wa mchezo huo ilionesha uhai kwa kuwashambulia wapinzani wao na kumiliki vyema mpira lakini walipata tabu katika umaliziaji.
Dakika mbili baada ya kufungwa bao la kwanza, Pacome Zouazou aliingia ndani ya eneo la penalti na kujaribu kuwapunguza mabeki wa CR Belouizdad kabla ya Mamadou Samake kumkwatua yeye na mpira lakini mwamuzi akapeta.
Yanga ilifanya shambulizi lingine dakika ya 20 baada ya Mamadou kupoteza mpira katika eneo la hatari la Belouizdad na Maxi Nzengeli kufumua shuti la kimo cha mbuzi lakini kipa Alex Guenduz alikuwa makini na kuudaka mpira huo.
Kipindi cha pili Yanga iliongeza kasi ikiongezewa nguvu na Clement Mzize aliyeingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya na dakika ya 63, Mzize aliiwahi pasi ya Stephane Aziz Ki na kutaka kuudokoa mpira kwa lengo la ‘kumvisha kanzu’ kipa Guenduz ambaye hata hivyo alikuwa makini na kuudaka mpira huo wa juu.
Dakika ya 73, Aziz Ki aliuwahi mpira uliookolewa kwa kichwa na beki wa Belouizdad na kujipinda kwa shuti kali la mguu wa kushoto ambalo hata hivyo halikuwa na madhara ingawa liliwashtua mashabiki wa CR Belouizdad.
Katika kuimarisha kikosi cha Yanga, kocha Miguel Gamondi pia aliwatoa Aziz Ki na kumuingiza Hafiz Konkoni na Kennedy Musonda ambaye nafasi yake aliingia Moloko, mabadiliko ambayo hayakuweza kuisaidia timu hiyo.
Katika kundi la Yanga pia kuna timu za Al Ahly ya Misri na Mediama ya Ghana ambapo mechi inayofuata, Yanga itakuwa na kibarua kingine kigumu mbele ya Ahly.
Kimataifa Belouizdad yaipiga Yanga 3-0
Belouizdad yaipiga Yanga 3-0
Read also