Na mwandishi wetu
Aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametangazwa kuwa kocha mkuu mpya wa Polisi Tanzania akirithi mikoba ya Mrundi, Joslin Bipfubusa aliyeachia ngazi wiki chache zilizopita.
Uongozi wa Polisi Tanzania ulieleza kumpa Zahera kibarua hicho leo Ijumaa baada ya mazungumzo na tathmini ya kina kwa lengo la kuipa mafanikio timu hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Zahera amepewa mkataba wa miezi sita na tayari leo ametambulishwa katika kikosi cha timu hiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC Bara ikiwa na pointi tisa tu baada ya mechi 14.
Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo amepewa nafasi hiyo baada ya hivi karibuni kumaliza
mkataba wake Yanga kama mkurugenzi wa kukuza soka la vijana katika klabu hiyo ambayo kabla ya hapo alikuwa ndiye kocha mkuu.
Polisi ilimuondoa Malale Hamsini na kumleta Joslin aliyedumu kwa miezi mitatu tu, akiiongoza
timu hiyo katika mechi tisa na kuambulia pointi tano baada ya kushinda mechi moja, sare mbili na
kufungwa mechi sita.
