Rio de Janeiro, Brazil
Neymar Jr amekiri kuvuka mipaka kwa kitendo chake cha kumpiga kofi mchezaji mwenzake wa Santos, Robinho Jr na amemuomba radhi mchezaji huyo.
Uongozi wa klabu ya Santos ulianza kufanya uchunguzi wa tukio hilo baada ya Robinho Jr ambaye ndio kwanza ana miaka 18 kudai kuwa alipigwa usoni (kofi) na Neymar Jr baada ya kumpiga chenga.
Kitendo cha Neymar kuomba radhi kimefuta utata uliojitokeza kuhusu tukio hilo ambalo lilitokea wakati wachezaji wa Santos wakiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Rei Pele.
Neymar, 34 alijitokeza mbele ya vyombo vya habari Jumanne Mei 5, 2026 na kuomba radhi kwa tukio hilo lililotokea mwishoni mwa wiki wakati wachezaji wa Santos wakiwa katika mazoezi yao ya kawaida.
“Kama mnataka niombe radhi mbele ya vyombo vya habari, hivyo ndivyo na mimi nipo hapa,” alisema Neymar, mshambuliaji anayeshika rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye timu ya taifa ya Brazil (mabao 79).
Neymar Jr ambaye pia amewahi kuzichezea timu za Barcelona na PSG, akiwa uwanjani Jumanne katika mechi dhidi ya Recoleta iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, alishangilia kwa kumkumbatia Robinho Jr.
Robinho Jr ni mtoto wa Robinho, nyota wa zamani wa timu za Santos, Real Madrid, Man City na AC Milan ambaye pia aliwahi kucheza na Neymar Jr kwenye timu ya taifa ya Brazil.
“Nilivuka mipaka kwa nilichokifanya, hali ingeweza kuwa kivingine lakini nilijivuruga, kila mtu anafanya kosa, ndio ni kosa langu, kidogo nilifanya kosa,” alisema Neymar Jr.
Neymar Jr pia alisema Robinho Jr ni kijana anayempenda na anavutiwa naye kwa namna ya kipekee lakini katika soka huwa inatokea wakati mnajibizana na rafiki wakati mwingine hata ndugu yako.
