Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Frolent Ibenge ameridhishwa na ushindani alioupata dhidi ya Azam walipokutana juzi licha ya timu yake kupata ushindi mdogo wa bao 1-0.
Hilal walivaana na Azam katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wao wa pili wa kirafiki tangu watue Tanzania baada ya awali kuumana na Namungo.
Ibenge alisema alikuwa hawafahamu vizuri wachezaji wa Azam lakini ameona ubora walionao kulingana na changamoto za uwanjani walizompa huku akisifia kiwango chao akidai kinaweza kuwapeleka kwenye kilele cha msimamo wa ligi.
“Azam ni timu nzuri nilikuwa siwafahamu, wana wachezaji wazuri wengine naweza kuwachukua kwa timu yangu, inashangaza kuwaona hawako kwenye kilele cha msimamo lakini kwetu ilikuwa mchezo mzuri na wametoa ushindani mkubwa,” alisema Ibenge.
Kocha huyo aliongeza kuwa ingawa ugumu wa mechi hizi unaweza kuzalisha majeruhi kwenye kikosi chake lakini anaamini kipimo anachokipata pia ni bora zaidi kuelekea kwenye mechi yao ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.
Naye Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe alisema wameonesha kiwango kizuri katika mechi hiyo ukizingatia wamecheza na timu kubwa inayoshiriki michuano mikubwa Afrika hivyo imewapa mwanga kuelekea mchezo wao ujao wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.
“Nadhani tunastahili pongezi kwa mechi nzuri, ilikuwa wakati mzuri kucheza na Hilal katika mechi ya kirafiki na kuona namna gani timu imepambana na kuwa kipimo kizuri kujiandaa na Dodoma Jiji kwenye mechi ijayo.
“Hata wachezaji wao nadhani wamepata mechi nzuri kuelekea mchezo wao ujao kwa hiyo kwetu ni fahari kucheza na timu miongoni mwa wababe wa Afrika na wanacheza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Ibwe.
Hilal itakamilisha ziara yake nchini kwa kuvaana na Simba kwenye mechi itakayopigwa Januari 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.