Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema kwamba klabu hiyo imemhakikishia kuwa ataendelea na majukumu yake licha ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya nusu fainali.
Ancelotti (pichani) ambaye msimu uliopita aliiwezesha Real Madrid kutwaa taji la ligi hiyo kubwa barani Ulaya, kwa siku za karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kuinoa timu ya Taifa ya Brazil.
Baada ya Real Madrid kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Man City, zimekuwapo habari kwamba uongozi utaachana na kocha huyo lakini sasa mwenyewe amesema kitu hicho hakipo na ataendelea na majukumu yake kama kawaida.
“Kila mtu anajua jinsi mambo yangu yalivyo, nina mkataba hapa ambao unafikia mwisho mwaka 2024 na nataka kuendelea kubaki hapa,” alisema Ancelotti na hata alipoulizwa kama amehakikishiwa hilo alijibu, ‘ndio’.
Kocha huyo Mtaliano awali aliinoa Real Madrid kwa miaka miwili kati ya mwaka 2013 na 2015 na kuondoka akiwa ameipa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka mmoja kabla.
Alirudi kwa mara nyingine katika klabu hiyo Juni 2021 baada ya kuachana na Everton na kwa mara nyingine aliipa taji la 14 la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini safari hii amekwamia nusu fainali.
Ancelotti pia amekwama nchini Hispania baada ya Barca ambao ni mahasimu wa Real Madrid kubeba taji la La Liga wakiwa na mechi nne mkononi na wameiacha nyuma Madrid kwa tofauti ya pointi 14.
“Ungeweza kuwa msimu mzuri lakini haujawa msimu mbaya, ni kweli hatujaridhika hata kwenye La Liga lakini tulipambana hadi mwisho,” alisema Ancelloti.