Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga, umeahidi kumpa Rais Samia Suluhu Hassan zawadi ya kutimiza miaka miwili katika uongozi wake kwa kushinda mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir na kutinga hatua ya robo fainali.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D, na ikishinda mchezo huo wa keshokutwa Jumapili itakuwa imejihakikishia kucheza hatua ya robo fainali nyuma ya wapinzani wao Monastir ambao ndio vinara wa kundi hilo.
Rais wa Yanga, Hersi Said ameeleza kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yamekamilika ikiwemo kutimiza kila kitu kwa wachezaji wao na benchi la ufundi, lengo likiwa ni kuwapa ari wachezaji wao ili wapate ushindi katika mchezo huo.
“Huu ni mchezo mgumu ambao tunalazimika kupata pointi tatu, nashukuru kocha Nasreddine Nabi na vijana wake wametuahidi ushindi kutokana na maandalizi aliyofanya kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Hersi.
“Lengo letu ni kumpa zawadi ya kutimiza miaka miwili Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri iliyotukuka,” alisema Hersi.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze ameeleza namna walivyokiandaa kikosi chao kwa ajili ya mchezo huo huku akisema wanachohitaji ni ushindi ambao utawahakikishia nafasi yao ya kwenda robo fainali kabla ya mechi ya mwisho.
Alisema wachezaji wao wote wapo fiti na wameonesha ari kubwa na wao kama benchi la ufundi kazi yao ya kurekebisha makosa madogo madogo yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita wameikamilisha na kilichobaki ni muda wa mchezo kufika ili kupata kile walichokikusudia.
Yanga ikishinda mchezo huo itafikisha pointi 10 ambazo zitawahakikishia kucheza robo fainali huku ikiwa imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya TP Mazembe ambao hata ikitokea wamefungwa matokeo hayawezi kuathiri safari yao ya kucheza hatua inayofuata.