Paris, Ufaransa
Aliyekuwa kocha wa Crystal Palace, Patrick Vieira (pichani) yuko mbioni kukabidhiwa jukumu la kuinoa klabu ya RC Strasbourg inayoshiriki Ligi 1 nchini Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu.
Vieira, kiungo wa zamani wa Arsenal, Machi mwaka huu alitimuwa Crystal Palace inayoshiriki Ligi Kuu England (EPL) na sasa anajiandaa kumrithi Frederic Antonetti aliyeinusuru Strasbourg kushuka daraja.
Mpango mzima wa Vieira kuinoa timu hiyo umefanikiwa baada ya wamiliki wa klabu ya Chelsea kununua hisa nyingi katika klabu ya Strasbourg ambayo msimu uliopita ilimaliza Ligi 1 ikiwa nafasi ya 15, ikikwepa janga la kushuka daraja kwa tofauti ya pointi tano.
Vieira alianza kazi ya ukocha mwaka 2011 baada ya kustaafu soka la ushindani akiwa Man City ambapo mwaka 2013 alianza kufundisha timu za vijana wadogo katika klabu hiyo.
Mwaka 2015, Vieira ambaye pia alikuwamo katika kikosi cha Ufaransa kilichobeba taji la dunia mwaka 1998, alikuwa kocha wa New York City FC ya Marekani kabla ya kurudi Ulaya miaka mitatu baadaye na kuwa kocha wa klabu ya Nice ya Ligi 1 nchini Ufaransa.
Aliiongoza vyema Nice ambayo ilimaliza nafasi ya saba kabla ya kutimuliwa Desemba 2020 na Julai 2021 alirudi England na kuanza kuinoa Palace akichukua nafasi ya Roy Hodgson.
Vieira mwenye umri wa miaka 47, alitimuliwa Palace Machi mwaka huu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ingawa ana rekodi ya kuifikisha nusu fainali ya Kombe la FA.
Kimataifa Vieira kuwa kocha mkuu Strasbourg
Vieira kuwa kocha mkuu Strasbourg
Related posts
Read also