Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ (pichani) amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu usajili akisema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato huo.
Dirisha dogo la usajili limefunguliwa tangu Desemba 15, mwaka jana na linatarajiwa kufungwa Januari 16, mwaka huu, hadi sasa Simba imekamilisha usajili wa mchezaji mmoja kati ya sita iliyokusudia kuwasajili kwenye dirisha hili.
Try Again alisema ukimya wao unatokana na kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya taratibu za usajili kwa wachezaji ambao wamepanga kuwasajili waliopendekezwa na kocha wao mkuu, Abdelhak Benchikha.
“Mashabiki wetu wasitishike na kelele za majirani kwa kutambulisha wachezaji wapya, usajili tunaokwenda kuufanya kwenye dirisha hili dogo unahitaji umakini mkubwa kutokana na malengo tuliyonayo, ndio maana tumekuwa kimya tukikamilisha baadhi ya taratibu kabla ya kuwatambulisha,” alisema Try Again.
Kiongozi huyo alisema pamoja na ugumu uliopo lakini mwanzoni mwa wiki ijayo watatambulisha nyota wawili kwa pamoja na baada ya hapo watamalizia wachezaji wengine siku mbili kabla dirisha kufungwa.
Mashabiki wa Simba wamekuwa na hofu kutokana na ukimya wa uongozi wao na hiyo imekuja baada ya wapinzani wao Yanga kumtambulisha Augustine Okrah raia wa Ghana.
Azam FC nao wametambulisha wachezaji wawili wapya, mshambuliaji wa Colombia, Franklin Navarro na kipa Mohamed Mustafa kutoka Sudan huku Simba wao wakimtamtamulisha Selehe Karabaka kutoka JKU ya Zanzibar.