Rio de Janeiro, Brazil
Shirikisho la Soka Brazil (CBF) sasa litakuwa na haki ya kutoa adhabu kwa timu ambayo mwajiriwa au shabiki wake atahusika na kosa la ubahuzi wa rangi ikiwamo kuinyang’anya timu pointi.
Sheria hiyo ambayo imeidhinishwa na klabu 20 za daraja la kwanza, ni sehemu ya mkakati wa CBF katika kukabiliana na dhihaka zinazoandamana na kauli za ubaguzi wa rangi kwenye viwanja vya soka.
Kwa mujibu wa CBF, sheria hiyo inatarajia kuanza kutumika Februari 22 wakati wa mashindano maarufu nchini Brazil ya Copa do Brazil.
“Vita dhidi ya ubaguzi wa rangi ni jambo lenye uharaka, suluhisho limekuwa mjadala kwa karne sasa lakini hakujawahi kuwa na utekelezaji, tumeamua kwenda mbele zaidi, tunaweza hata kuzinyang’anya timu pointi katika moja ya mashindano yanayoratibiwa na CBF,” alisema Rais wa CBF, Ednaldo Rodrigues.
Akiwa ndiye mtu wa kwanza mweusi mwenye asili ya Afrika kuongoza CBF katika kipindi cha zaidi ya miaka 100, Rodrigues anaichukulia vita dhidi ya ubaguzi wa rangi kwenye oka kuwa moja ya kipaumbele chake kikuu.
CBF inakuwa mamlaka ya kwanza duniani kuja na sheria ya aina hiyo kwa lengo la kukabiliana na ubaguzi wa rangi kwenye soka.
Rais wa Brazil, Lula da Silva amepitisha sheria inayolitaja kosa la dhihaka za kibaguzi kuwa ni kosa la jinai na kuongeza adhabu kosa hilo linapofanyika kwenye viwanja vya michezo au hafla za utamaduni nchini Brazil.
Tatizo la ubaguzi wa rangi hasa kwenye viwanja vya soka limekuwa kubwa zaidi barani Ulaya ambapo katika siku za karibuni mchezaji wa Brazil anayeichezea Real Madrid, Vinicius Junior amejikuta katika kadhia hiyo.
Vinicius aliwahi kusema kwamba tatizo linakuwa kubwa kwa sababu hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaohusika kufanya vitendo hivyo.