Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simon Msuva ameshukuru kupatikana kwa haki yake aliyokuwa akiipigania kutoka klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco na kueleza mengi aliyopitia alipokuwa na timu hiyo ambayo wengi hawayajui.
Msuva ameeleza hayo ikiwa ni takriban siku mbili zimepita tangu Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lilipoiamuru Wydad kumlipa mchezaji huyo Dola za Marekani 700,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.6 za Tanzania) ikiwa ni fidia ya malimbikizo ya mshahara wake na pesa za usajili.
Mchezaji huyo anasema utata ulianza baada ya kutolipwa pesa ya usajili kwa mafungu matatu ndani ya msimu wa kwanza kama walivyokubaliana awali badala yake kukawa na danadana juu ya hilo, kisingizio kikiwa ni janga la covid-19.
“Ukiangalia mshahara wangu haukuwa mkubwa ulikuwa mdogo na ndoto yangu kubwa ni kupata hela ya usajili ili nifanye kitu lakini ikawa siyo vile na ukiongea nao kikubwa wanasema janga la corona.
“Sawa ni Corona lakini pia hakukuwa na mawasiliano mazuri kati yangu na rais wa timu kwa sababu aliingia kwenye siasa, kugombea ubunge. Muda mwingi hakuwa karibu na timu, hajui wachezaji wanaishije na hilo halikuwa kwa upande wangu tu, wengine wa palepale pia walikuwa wanadai,” alisema Msuva.
Alisema kuwa hali hiyo hakuifurahia, kwa sababu kwenye timu alikuwa anatumika, anafunga na kutoa pasi za mabao hivyo ilikuwa lazima apambanie haki yake akishirikiana na wakala wake na kusisitiza kuwa hakuondoka Morocco kwa kukata tamaa ila alikuwa akipigania haki yake.
“Kocha alikuwa karibu na mimi, kwa sababu alikuwa ananitumia, ananipenda, ilifika kipindi watu hawajui tu lakini alikuwa ananipa hela ya kulipa maji, umeme ndani nilikuwa sina na Watanzania hawajui hilo, wanaona mbona naishi vizuri tu.
“Wajue kuna wakati nje ya nchi kuna changamoto nyingi unapitia siyo kila changamoto utaisema lakini vingine inabidi uvisema ili watu wajue kwamba kweli kuna changamoto, mimi sikukata tamaa, niliondoka kwa sababu ya kufuata sheria,” alifafanua Msuva.
Mshambuliaji huyo ameeleza kiasi kilichoelekezwa na Fifa alipwe anastahili kutokana na kiwango kikubwa cha ada yake ya usajili wakati anajiunga na timu hiyo akitokea Difaa El-Jadida msimu wa 2020/21 huku akifafanua kama watashindwa kulipa pesa hizo ndani ya wiki mbili basi kiasi hicho kitaongezeka.
“Kwa sababu ada yangu ya usajili ilikuwa kubwa inafika kwenye kiasi hicho na nafikiri wamepewa kama siku 15 walipe la sivyo watapigwa penalti, hela itaongezeka na mimi nataka iongezeke.
“Iongezeke kwa sababu sisi watu weusi tuna njaa, halafu tunadhulumiwa sana halafu tuna vipaji. Mara nyingi Mungu ndiyo anatuokoa lakini tunapitia magumu sana, namwaga jasho langu, kuna wakati nilikuwa naumwa nyonga lakini nafungwa bandeji, nachomwa sindano ilimradi niitumikie timu na hakuna anayejua.
“Sasa hayo ndiyo malipo yangu, kwa sababu rais (wa timu) alikuwa anadanganya umma kwamba amenilipa simdai lakini sasa imeonekana na watu wamejua kwamba kweli Simon alikuwa anadai na alikuwa na haki na imetangazwa na sasa Watanzania wote wamejua Msuva hakuwa na makosa,” alihitimisha Msuva.
Desemba, mwaka jana Msuva alivunja mkataba wake wa miaka minne na Wydad akishinikiza kulipwa stahiki zake na kurejea nyumbani kabla ya majuzi kutangazwa mshindi wa kesi hiyo.
