Jakarta, Indonesia
Chama cha Soka Indonesia (PSSI) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa pamoja wataunda kikosi kazi kwa lengo la kuboresha udhibiti wa mashabiki na usalama kwenye mechi za soka baada ya kutokea vifo vya mashabiki zaidi ya 130 kwenye mechi ya soka mapema mwezi huu.
Vifo hivyo vilitokea baada ya mashabiki wa timu ya Arema FC kuvamia uwanjani mara tu baada ya mechi na mahasimu wao Persebaya Surabaya kumalizika wakati huo Surabaya wakiwa wanaongoza kwa mabao 3-2.
Mamlaka nchini Indonesia kwa sasa zinahaha kutafuta namna ya kufumua mfumo mzima wa usalama katika mechi za soka baada ya vifo vya mashabiki hao vilivyotokea Oktoba Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Kanjuruhan, East Java hilo likiwa tukio kubwa la vifo kwenye historia ya soka nchini humo.
Wataalam wa mambo ya usalama nchini humo walisema kwamba kitendo cha polisi kutumia mabomu ya machozi kutawanya mashabiki wa timu ya Arema FC ndiyo chanzo cha vifo hivyo. Fifa imepiga marufuku matumizi ya mabomu ya machozi kwenye viwanja vya soka.
“Tumekubaliana kuunda tume au kikosi kazi kitakachofanya maboresho ya mfumo wa usalama kwenye viwanja vya soka, kikosi kazi kitajumuisha watu kutoka serikalini, Fifa na wataalamu wa soka, maofisa wa afya, wanausalama, maofisa wa wizara ya michezo na wasimamizi wa viwanja vya soka,” alisema kiongozi wa PSSI, Mochamad Iriawan mara baada ya kikao na maofisa wa Fifa.
Kwa mujibu wa Iriawan katika mpango huo, polisi nchini Indonesia watatakiwa kuhakikisha mfumo wao wa usalama kwenye viwanja vya soka unafanyiwa mabadiliko ili kuendana na taratibu zinazokubaliwa na Fifa.
Rais wa Indonesia, Joko Widodo alisema kwamba Fifa haijawa na mpango wa kuifungia Indonesia kwa sababu ya tukio hilo lakini uamuzi wa shirikisho hilo kuingilia kati ni kwa kuwa Indonesia inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 20 mwakani.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino anatarajia kwenda Indonesia Jumanne ijayo ambapo pamoja na mambo mengine anatarajia kukutana na Rais Widodo na baada ya kikao hicho wajumbe wa kikosi kazi pia watatangazwa.
Watu sita wakiwamo polisi na waandaaji wa mechi hiyo wamekamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya jinai baada ya tukio hilo ambapo taarifa ya Serikali ilidai kuwa kufungwa baadhi ya milango ya kutokea na mashabiki kujaa uwanjani kuliko idadi inayotakiwa ni kati ya sababu zilizochangia vifo hivyo.
Kimataifa Fifa yaingilia kati vifo vya mashabiki Indonesia
Fifa yaingilia kati vifo vya mashabiki Indonesia
Read also