Manchester, England
Manchester City hatimaye imekamilisha usajili wa kiungo wa Croatia, Mateo Kovacic kutoka klabu ya Chelsea kwa ada inayotajwa kufikia pauni 25 milioni.
Kovacic mwenye umri wa miaka 29 na ambaye amesaini miaka minne ndio usajili wa kwanza wa timu hiyo tangu kumaliza msimu na mataji matatu ingawa inadaiwa kwamba huenda ada yake ikaongezeka.
Man City imekamilisha usajili wa mchezaji huyo ikiwa ni siku chache baada ya kutangaza kuondoka kwa kiungo Ilkay Gundogan ambaye amejiunga na Barcelona akiwa mchezaji huru.
Baada ya kumpata Kovacic, Man City kwa sasa inapambana na Arsenal katika kuiwania saini ya kiungo wa West Ham, Declan Rice na tayari ofa yao ya Pauni 90 milioni imekataliwa.
Kovacic alitua Chelsea Agosti 2018 akitokea Real Madrid, katika msimu uliopita wa 2022-23 ambao ulikuwa mbaya kwa timu hiyo iliyomaliza ligi ikiwa nafasi ya 12, mchezaji huyo amecheza mechi 37.
“Hii ni hatua kubwa kwangu, na sina cha kusubiri kabla ya kuanza msimu nikiwa na City,” alisema Kovacic ambaye habari za kutakiwa na Man City zilianza kusikika takriban siku 10 zilizopita.
“Yeyote ambaye ameiangalia timu hii chini ya Pep (Guardiola) anajua namna ilivyo vizuri, kwangu mimi hii ni timu bora duniani, mataji waliyoshinda yapo wazi kwetu sote lakini pia ni timu bora ya soka,” alisema Kovacic.