Bremen, Ujerumani
Nahodha wa England, Harry Kane kwa mara ya kwanza jana Ijumaa aliifungia bao timu yake mpya ya Bayern Munich iliyoipata ushindi wa 4-1 dhidi ya Werder Bremen katika mechi ya Ligi ya Bundesliga.
Kane aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni kwa ada ya Pauni 86.4 milioni akitokea, Tottenham, alifunga bao hilo dakika ya 74 kwa shuti hafifu la mguu wa kulia la umbali wa mita 15 lililomsinda kipa wa Bremen, Jin Pavlenka.
Bao hilo la Kane lilikuwa la pili na kabla ya hapo ndiye aliyetoa pasi kwa Leroy Sane iliyozaa bao la kwanza mapema katika dakika ya nne ya mchezo.
Mabao mengine mawili ya Bayern yalipatikana katika dakika nne za nyongeza, la kwanza likifungwa na Sane kwa mara nyingine na la mwisho likifungwa na Mathys Tel.
“Nilikuwa mwenye hali ya wasiwasi na hapo hapo furaha ya kucheza mechi hii, tulianza vizuri na kupata goli katika dakika chache za awali, hakika kulikuwa na hali tete kidogo lakini wakati wote ninapokuwa uwanjani, fikra sahihi huchukua nafasi yake,” alisema Kane.
Kane alijikuta akiwa mjadala baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na timu hiyo lakini akashindwa kuisaidia ilipokutana na kipigo cha mabao 3-0 mbele ya RB Leipzig katika mechi ya Super Cup Ujerumani.
Bayern inaamini Kane anaweza kuwa mabadala wa mpachika mabao wao mahiri, Robert Lewandowski aliyehamia Barcelona wiki kadhaa kabla ya kuanza kwa msimu uliopita wa 2022-23.