Roma, Italia
Kocha wa Roma, Jose Mourinho ambaye ana wakati mgumu katika timu hiyo, amesema kwamba anaamini atakwenda kufundisha soka Saudi Arabia.
“Nitakwenda Saudi Arabia nikiwa na muda wa mapumziko, lakini naamini kwamba nitakwenda pale kufanya kazi, sijui lini lakini nina uhakika na hilo,” alisema Mourinho.
Mourinho aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifanya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha nchini Misri ambacho kinamilikiwa na kampuni ya Saudi Arabia.
“Hakuna anayeyajua mambo ya baadaye, lakini nitalifanya hilo (kwenda Saudi Arabia), sijui lini,” alisema Mourinho ambaye pia ni kocha wa zamani wa Chelsea.
Mourinho, 60, alisema hivi karibuni kwamba alikataa ofa nono ya kufanya kazi Saudi Arabia ili aendelee kuinoa Roma kwa msimu wa tatu baada ya kuiwezesha kutwaa taji la Uefa Conference Ligi na kuifikisha fainali ya Europa Ligi msimu uliopita.
Kocha huyo alitua Roma kwa mara ya kwanza Mei 2021 na kujipatia mafanikio katika misimu miwili iliyopita ingawa msimu huu umeonekana kuwa mgumu kwake.
“Milango ipo wazi kwangu kwa wakati wote kule Saudi Arabia, nataka kuona hali ya maendeleo ya pale, Cristiano (Ronaldo) ni wa kwanza kwenda pale na kuleta utofauti haraka, wachezaji awali walidhani lingekuwa tukio la mtu mmoja lakini kwa haraka kila kitu kikabadilika,” alisema Mourinho.
Mourinho ambaye amewahi kutwaa mataji kadhaa, pia amewahi kuzinoa timu za FC Porto ya Ureno, Real Madrid ya Hispania, Inter Milan ya Italia pamoja na Man United na Tottenham za England.