Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema kwamba mmiliki mwenza wa klabu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe anatakiwa kuwa makini ili asivuruge maendeleo yaliyofanywa na klabu hiyo katika kipinid cha kocha huyo.
Ratcliffe na kamapuni yake ya INEOS, ameanza kufanya mabadiliko kadhaa ikiwamo kumuajiri Omar Berrarda katika nafasi ya Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na wanadaiwa kuwa mbioni kuwaajiri, Jason Wilcox na Dan Ashworth katika majukumu ya msingi ya ukuzaji wa vipaji.
Ten Hag, 54, kocha kutoka Uholanzi ametoa kauli hiyo wakati huu kukiwa na uvumi kwamba menendo usiovutia wa timu hiyo unaweza kuwa sababu ya kocha huyo kutimuliwa mara baada ya msimu huu.
Pamoja na uvumi huo, Ten Hag ambaye ana mkataba hadi mwaka 2025 ameonesha dalili zote za utayari wa kutaka kuendelea kuwa na timu hiyo hadi msimu ujao.
“Nafikiri unahitaji kufuata mfumo, tuna wachezaji wazuri vijana walioingia, wapo katika mfumo na wanaendelea vizuri, tuko vizuri, katika mwelekeo mzuri na tunahitaji kwenda hatua inayofuata, usivuruge huu mfumo,” alisema Ten Hag.
Man United Alamisi hii itakuwa uwanjani kukabiliana na Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) ikijaribu kufuta makosa baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Brentford katika mechi ya Jumamosi iliyopita.