Na mwandishi wetu
Simba imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuipa kipigo kikali cha mabao 6-0, Jwaneng Galaxy katika mechi iliyopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba kufuzu hatua hiyo ikiwa na pointi tisa na kuungana na Yanga na hivyo kuifanya Tanzania kwa mara ya kwanza kuwa na timu mbili katika hatua hiyo.
Karamu ya mabao ya Simba ilianzia dakika ya saba ya mchezo huo kwa bao lililofungwa na Saido Ntibazonkiza na dakika saba zilizofuata Jwaneng walijikuta wakipachikwa bao la pili lililofungwa na Pa Omar Jobe.
Mambo yaliendelea kuwaharibikia Jwaneng baada ya dakika nyingine saba walipojikuta wakifungwa bao la tatu lililojazwa wavuni na Kibu Denis na kuzifanya timu ziende mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao matatu.
Baada ya kuingia mabao Jwaneng walijaribu kufurukuta lakini hawakufanya shambulizi lolote la maana langoni mwa Simba badala yake ni Simba waliokosa mabao mawili ambayo yote yalitokana na mashuti ya chini ya Clatous Chama yaliyogonga mwamba.
Mashambulizi hayo yalimfanya kipa wa Jwaneng, Phoko kuwalaumu mara kwa mara mabeki wake kwa namna walivyogeuzwa uchochoro na safu ya ushambuliaji ya Simba.
Kipindi cha pili Simba waliendelea na kasi ya mashambulizi na kuandika bao la nne dakika ya 76 lililofungwa na Chama ambaye aliitumia pasi ya Saidoo ambaye aliunganishiwa pasi ndefu na Donald Ngoma.
Simba iliandika bao la tano dakika ya 81 lililofungwa na Chasambi ambaye aliitumia pasi ya Fred Michael wakati bao la sita na la mwisho lilifungwa muda mfupi baadaye na Ngoma aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa akiitumia pasi ya Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Kimataifa Simba yailaza Jwaneng 6-0, yatua robo fainali
Simba yailaza Jwaneng 6-0, yatua robo fainali
Read also